Hotuba Final[1]
Transcript of Hotuba Final[1]
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
1/24
1
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2013
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza
nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila
mwisho wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu
ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping,
Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya nchini
kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. Lengo la
ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria
uliopo kati ya China na Tanzania. Napenda kuchukua
nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa
kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake.
Wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi
yetu na watu wake.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
2/24
2
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani
kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa na
mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee
kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni
wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za
usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa XiJinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara
ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi
yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na
kumbukumbu isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi
ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu
baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na,
kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini
kutangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika
kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika
bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi wapya
wa China. Pia, kuwa China itaendelea kukuza biashara
na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa
Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
3/24
3
vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi zetu mbili
zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja
mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu
ya kipaumbele nayo imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na kusisitiza dhamira yake
na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti cha China ya
kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati yaTanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo
ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi zetu, yaani
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa
kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong
aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri Mkuu
wake Chou En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa nchi yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa na
kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo
kwa kuongeza misaada ya maendeleo. Katika miaka
49 ya uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu
imepata misaada mingi ya maendeleo ikiwemo Ukumbi
wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao
ulizinduliwa na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
4/24
4
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa inayoendelea
kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada waSerikali ya China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi Jinping
iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya
maendeleo kama tulivyoomba wakati wa mazungumzo
yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la GhorofaJijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya
kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa
linajengwa katika jiji la Dar es Salaam. Ajali hiyo
iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na
simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu
30 zimepatikana. Watu 17 waliweza kuokolewa,
wanne kati yao bado wanaendelea na matibabu katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na
kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea
na sasa inakaribia kufikia ukingoni.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
5/24
5
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya
kwenda kuangalia eneo la ajali. Hali niliyoiona paleimenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata hivyo,
kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za
uokoaji zilizokuwa zinafanywa na wanajeshi wetu
wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na
wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani
maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu
Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia
nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond
Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na
askari wa JWTZ, na wale wote walioshiriki na
wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali nyinginezo
kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya waliojeruhiwa.
Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu
na jamaa zao katika ajali hii. Nawaomba wawe na
moyo wa subira huku sote tukiungana nao kuwaombea
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
6/24
6
marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.
Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha
ajali ile. Alimradi kila mtu ana dhana yake. Niliagiza
vyombo na mamlaka husika wachukue hatua zipasazo
kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na
watakaothibitika kusababisha maafa hayowachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa
Mahakamani washitakiwe na wa kufutiwa leseni za
kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao wafutiwe
bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa
mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima
zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini kama
mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali
hii ingeepukika. Halmashauri za miji na wilaya zina
wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao.
Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe
fundisho kwa wote.
Ndugu Wananchi;
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
7/24
7
Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa
Wakandarasi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi
itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli
ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na
Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao
washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na
hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna
bora ya kukomesha ajali za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo
ni uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini. Jambo
hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma,
lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo
sasa. Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na
waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali kubadili
muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu
nzuri tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya
Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa
upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka.
Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
8/24
8
katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi
wa dini za Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini
haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo
mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande
unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwinginekwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na
mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi
vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada,
mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa
dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa
kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu
kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo
inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha,
Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na
Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo
wanadai kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia
wake. Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea
upande wa Waislamu.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
9/24
9
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao
kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwakuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo
na Serikali haichukui hatua yo yote ya maana.
Waislamu wananyanyaswa katika nchi yao,
wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba
Serikali inawapendelea Wakristo. Wanasema nchi
inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi
wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi
kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama
vile harambee za kujenga Makanisa na shule za
Makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko
ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo Misikiti
mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife.
Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali
wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu
kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
10/24
10
upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu
kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo
wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya
Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa
nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua
wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu
tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera
na maelekezo yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa
mara kadhaa nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na
Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha ajizi
katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za
Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose
nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli
nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume
Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na
madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi
ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu
mbalimbali Waislamu na Wakristo. Pale ambapo
sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa
sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
11/24
11
lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda mfupi.
Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara
mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa
ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu
za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda
pengine siyo nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo,
huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu
haijashindwa kulinda usalama wa raia wake au viongozi
wa dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa hivyo,
tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na
matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi
hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana ndugu
zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie
matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila
kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule
Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili
Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri
Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa
Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
12/24
12
na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu
wake.
Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wavyombo vya Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa
matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa hatujapata
ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga
kuua viongozi wa Kikristo na kuchoma moto Makanisa
hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere
ni matokeo ya vurugu zilizosababishwa na mzozo kati
ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye
bucha iliyopo pale kijijini ambayo kwa mazoea huuzwa
nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na
vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote
walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha. Si tukio
unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale
pale Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha
Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu zao.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
13/24
13
Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile
kuuzwa katika bucha ile kuumizana kule na mauaji yale
yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na Waislamu
wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao.
Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana katika
shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja
akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo
kutumia tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa
kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa
Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni
kulikuza tatizo isivyostahili. Busara ituongoze kutafuta
njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa
Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee
kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali. Hata mzozo wa
kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za
kitimoto zipo na watu hawajapigana. Kutumia mzozo
wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo na
Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei haki
Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni
tukio linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
14/24
14
Buseresere, Geita. Hapakuwa na mzozo kuhusu nani
achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na
tumehusisha vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane
na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya hivyo kwa
sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa
matukio ya kabla yake. Yaani ile la kupigwa risasi na
kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa
tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili
Soroga. Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na
bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu
yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule
Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale
matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua
fumbo hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu
nzuri. Lakini inabaki kuwa ni dhana ya kibinadamu
mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya
uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya
usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wanje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno
kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali
ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
15/24
15
Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina
sababu ya kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika
usiku na mchana kupata jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar
Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na
kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina
mazingira yake maalum. Chanzo chake ni mzozouliotokana na tukio la kusikitisha la kijana mmoja
Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani
Quran Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na
ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo
hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa
kituo cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo
mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana
wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa. Kukatokea
mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya
kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka pale,
wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na
kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
16/24
16
Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio
la kuchomwa Kanisa mahali popote kwa upande wa
Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la
watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno
ya vitisho vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa
kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila ujumbe wa
namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama
uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari
kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja
iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili
hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina
mbalimbali hupelekwa kote, kwa Wakristo na
Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia
wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo
wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa Wakristo wanao
mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu
nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu
wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha nakutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa
sababu wanazozijua wao na kwa faida yao.
Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
17/24
17
Waislamu wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya
Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane
Serikali imewatelekeza raia wake. Ni mchezo mbaya,
tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu
mmekaa chini na kujiuliza kumetokea nini kipya hata
leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na
Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya
uhalifu. Watu 76 wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma
moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo kituo cha
Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea
Mahakamani. Kwa upande wa tukio la Buseresere
lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila,
watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na
Kiislamu walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo
walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa
kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu
wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao
wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar, watu 10
wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na
kesi zao zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
18/24
18
tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada ya kuuawa
Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda,
bado uchunguzi haujakamilika pamoja na kuwapo
taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi. Kuhusu
uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada
kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchizilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya aina hii,
hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja
amekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako piaSerikali imechukua hatua. Watu kadhaa
wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika
maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na
kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za
kidini. Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu
wengine ambao wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa
kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la
Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
19/24
19
Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha nchini.
Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha
Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa
kwa muda wa miezi sita. Baada ya muda huo kupita,
Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano
itaamua ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwaSerikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na
amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe hatujashindwa
kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi
yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kuhakikisha
kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote, rangi
zote na mahali po pote walipo wako salama. Tunataka
kuona watu wanaendelea kuishi kwa amani, upendo,
ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi
siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka
mambo yanayowabagua na kusisitiza yale
yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele
yale yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
20/24
20
Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe
fundisho kwetu sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie maisha yetu
Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii
kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo
tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na
Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na
vyuo pawe na majiko mawili au labda hata mabwalo
mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini
nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na
Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na
maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu?
Tunataka kujenga nchi ya namna gani? Mimi naamini
tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa
kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa
kwa namna ambayo hatutakuwa wamoja tena. Huko
tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na wakati ni
huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushewaumini wao na taifa letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
21/24
21
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa
dini zetu kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii
na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu mwingine ye
yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala
yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi
wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao. Serikali ina
wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama
waumini hawatafanya vitendo vitakavyosababisha
uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na
lipi baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa
madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu
kuzungumza nao kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja
kuona kuwa wote wanasikitishwa na mambo
yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya viongozi
wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.
Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa
Tanzania na Watanzania. Kuna upepo mbaya wa
shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu
wa kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na
kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
22/24
22
tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa dini tofauti
wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano na
mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na
Utanzania wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda,
ameshaeleza dhamira ya Serikali ya kuitisha mkutano
wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao. Ni
matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila
ya kutuma wawakilishi. Lazima tupate jawabu kwa
maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia
nafasi hii kuwaomba na kuwasihi waandishi wa habari
wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita vya
kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na
kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu.
Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya
kuziandika au kuzitangaza. Wawe makini na maneno
wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa lazima sote
tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja
miongoni mwa Watanzania wa dini zote. Wasipofanya
hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
23/24
23
ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi
jirani. Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari
kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo
vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea
uhasama baina ya Wakristo na Waislamu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi
wote kudumisha umoja na mshikamano wetu. Tuishi
kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila
kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali
atokako mtu. Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania
ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na
kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali
haipendelei dini yo yote na wala haina mpango wa
kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao.
Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea
kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao
kama inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona
kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende
kutoa taarifa Polisi. Hatua zipasazo zitachukuliwa.
-
7/28/2019 Hotuba Final[1]
24/24
24
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka.
Tusherehekee kwa amani na utulivu. Tusherehekeepamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.