Ewe Muislamu,
Kumbuka Mauti!
´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aal
ash-Shaykh
Mfasiri:
Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush
©
Bismillaahi Rahmaani Rahiym
Mada ya leo ni kuongelea siku ya Aakhirah. Kwanza Allaah (Jalla wa ´Alaa)
Kafanya (nyumba) vituo vitatu; nyumba ya ´amali, nyumba ya malipo na
nyumba baina ya hizo mbili. Dunia yote ni nyumba ya kufanya ´amali bila ya
hesabu.
"Na sema: Tendeni vitendo. Na Allaah, na Mtume wake, na Waumini
wataviona vitendo vyenu." (09:105)
Ni nyumba ya ´amali, hakika Allaah (Ta´ala) Katuumba ili kumuabudu Yeye
mmoja asiyekuwa na mshirika. Na kusimama na ya wajibu ambayo
Kayawajibisha juu yetu; katika kumtakasia dini na kumpwekesha kwa kila
aina ya ´ibaadah na kutekeleza Shari´ah Yake na kusimama kwa hilo.
"Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika
ardhi ili tuone jinsi mtakavyotenda." (10:14)
Na Kaifanya Aakhirah kuwa nyumba ya malipo:
"... ili awalipe walio tenda ubaya kwa waliyoyatenda, na waliotenda mema
awalipe mema." (53:31)
Na kuna nyumba baina ya nyumba hizi mbili, dunia na Aakhirah nayo ni
Barzakh. Nayo ni kaburi anapolazwa mtu baada ya roho kutengana na mwili
wake mpaka Allaah Atapotoa idhini ya kuhesabiwa waja Ewe Muislamu!
Tumeumbwa katika dunia hii ili tupewe mitihani. Kama Asemavyo Allaah:
"Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ninani miongoni mwenu
mwenye vitendo vizuri zaidi." (67:02)
Katika uhai kuna mitihani, na katika mauti kuna mitihani. Kaumba Allaah
mauti na uhai ili atujaribu ni nani kati yetu mwenye matendo mazuri zaidi.
Katika mauti kuna balaa na mitihani. Kwa kuwa kuyakumbuka mara kwa
mara daima kunaufanya moyo kuwa sawa na kufanya juhudi ya ´amali njema
na kujitayarisha nayo [mauti] na yaliobaada yake.
Uhai ni balaa kwa mja, mja hupewa mitihani katika uhai wake. Je, atakuwa
mja mwenye kushukuru kumtimizia Allaah haki Zake au kinyume chake.
Hakika dunia hii ni upuuzi na mchezo na mapambo tu kama Alivyosema
Allaah:
"Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na
kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto."
(57:20)
Ataejua kuwa uhai wake umekadiriwa kwa zama ambazo Anazijua Mola
wetu, anatakiwa kujiandaa na yalio baada ya mauti. Na ajue kuwa akifanya
mchezo katika dunia hii na kupoteza muda wake, atajuta siku ya Qiyaamah:
"Isije ikasema nafsi: “Ee majuto yangu kwa yale niliyopoteza upande wa
Allaah, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara!” Au
ikasema: “Ingeli kuwa Allaah Ameniongoa, bila ya shaka ningelikuwa
miongoni mwa wenyekumcha Allaah”. Au ikasema inapo ona adhabu: “Lau
kuwa ningelipata fursa nyengine, ningelikuwa miongoni mwa wafanya
mema”." (39:56-58)
"Na lau ungeliona watavyosimamishwa mbele ya Mola wao, akawaambia: “Je,
si kweli haya?” Na wao watasema: “Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu ni
kweli”." (06:30)
Watatamani wakati huo warudishwe duniani ili watengeneze walipoharibu.
Anasema Allaah (Ta´ala) kuhusu wao:
"Na watasema: Lau kuwa tungelisikia, au tungelikuwa na akili, tusingelikuwa
katika watu wa Motoni!." Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu
wa Motoni!." (67:10-11)
Atatamani kurudishwa duniani huenda akatengeneza alipoharibu na kutimiza
ya wajibu kwake, lakini majito hayo hayatomfaa kitu. Ewe Muislamu! Hakika
Allaah Katuamrisha kujizidishia zawadi duniani kwa ajili ya Aakhirah yetu.
Akasema:
"Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni ucha Mungu. Na
nicheni Mimi, enyi wenye akili!." (02:197)
Hakuna atachojizidishia mja zaidi ya kumcha Allaah na ´amali njema, hakika
Allaah (Ta´ala) Hamdhulumu yeyote.
"Na anayetenda mema, naye ni Muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala
kupunjwa." (10:112)
Hatakhofu kudhulumiwa ikawa atabeba makosa ya wengine wala kupunjwa
mema yake. Bali mema yake yamehifadhiwa kwa ajili yake.
"Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa
ila sawa nao tu. Na wao hawata dhulumiwa.” (06:60)
Hakika uhai wa muumini ni haki alioamrishwa kumtii Allaah, kufanya khayr
na kujishugulisha kumtii Mola na akatumia siku zake, usiku wake, miezi yake
na miaka yake kujishughulisha na yatayomkurubisha kwa Allaah. Huku
akijua kuwa ´amali zote hizi zitahesabiwa kwake na kusimama kwazo na
huenda akazisahau.
"Siku atapowafufua Allaah, na awaambie yale waliyoyatenda. Allaah
Ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Allaah ni Mwenye kushuhudia kila
kitu." (58:06)
Ewe Muislamu! Hakika muumini katika uhai (maisha) yake ayaangalie kwa
mtazamo mzuri wa kuyapa umuhimu na kujishughulisha na
yatayomkurubisha kwa Allaah. Na mmoja wetu atapoteza muda wake katika
uhai huu akafanya maasi na maovu huku anaiona nafsi yake kuwa iko katika
usawa.
"Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao? Ni wale
ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani
kwamba wanafanya kazi nzuri." (18:103-104)
Allaah Katueleza kuwa Atatukusanya siku ambayo haina shaka ndani yake na
atatusimamishia ´amali zetu zote tulizofanya.
"Basi itakuwaje tutakapo wakusanya Siku ambayo haina shaka kuja kwake?
Na kila nafsi italipwa kama ilivyochuma, bila ya kudhulumiwa." (03:25)
Ewe Muislamu! Uhai wako umekadiriwa kwa zama ambazo zinajua Allaah,
elimu yake iko kwa Allaah:
"Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamah) kuko kwa Allaah. Na Yeye ndiye
anayeiteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na
haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi
gani. Hakika Allaah ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari." (31:34)
Ewe Muislamu! Hakika Muislamu anatakiwa daima amuombe Allaah
Amthibitishe katika Uislamu na Asiupoteze moyo wake baada ya kuuongoa.
Kwa kuwa anajua kuwa moyo wake uko baina ya vidole viwili katika vidole
vya Allaah; anaupeleka Apendavyo.
"Moyo za waja ziko baina ya vidole viwili katika vidole vya Allaah;
anazipeleka Apendavyo."
Ewe Muislamu! Tumeamrishwa kukumbuka mauti daima na milele. Allaah
Katukumbusha maslahi haya makubwa. Anasema Allaah (Jalla wa ´Alaa):
"Naye ndiye Allaah wa kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni
wa angalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha,
nao hawafanyi taksiri. Kisha watarudishwa kwa Allaah, Mola wao wa Haki.
Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu."
(06:61-62)
"Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha
mtarejeshwa kwa Mola wenu." (32:11)
"Popote mlipo mauti yatakufikieni, na hata mkiwa katika ngome zilizo na
nguvu." (04:78)
Na ni haki kuwa ajali yetu yatusubiri kama jinsi raziki zetu zatusubiri. Muda
wa mja unapoisha katika uhai wake aliomkadiria Allaah na kuupanga,
atafikwa na aliompangia Allaah. Na atajiwa na sakaratul maut na hali zake.
Anasema Allaah (Jalla wa ´Alaa):
"Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyokuwa
ukiyakimbia." (50:19)
Mja wakati anapoachana na dunia hii hukutana na mambo makubwa na hali
mbali mbali za kutisha, Lakini Allaah Huwathibitisha wale walio amini kwa
kauli iliothabiti katika uhai wa dunia na Huwapoteza Allaah madhalimu na
Hufanya Atakacho. Hakika ajali hii ikifikia wakati wake hakuna yeyote
awezae kuizuia.
Anasema Allaah (Ta´ala):
"Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha
mtarejeshwa kwa Mola wenu." (32:11)
Wakati roho inapotengana na mwili unafikwa na shida na khofu kubwa
zinazojua Allaah. Muislamu anapokuwa katika hali ya kuiaga dunia na
anaelekea Aakhirah huteremkiwa na Malaika wenye nyuso nzuri, nguo nzuri
nyuso zao kama jua. Kisha anajiwa na Malaika wa kutoa roho na kumwambia:
"Ewe ulie na nafsi nzuri, toka uje katika msamaha na radhi za Allaah; hapo
roho hutoka kwa upole na utaratibu.
Malaika wa mauti wanaichukua na kuiweka kwenye kafani waliokuja nayo
kutoka Peponi na harufu nzuri kama miski iliopatikana kwenye uso wa ardhi.
Wanapanda nayo [roho yake] mbinguni wanafunguliwa milango ya
mbinguni. Kila mbingu inasema:
"Hii ni roho ya fulani bin fulani kwa jina lake la duniani."
Anasema Allaah irudisheni katika ardhi:
"Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka
humo tutakutoeni mara nyengine." (20:55)
Itarudishwa roho kwenye mwili wake kisha ajiwe na Malaika wawili
wamuhoji; Mola wake, dini yake na Mtume wake.
Muumini atasema "Mola wangu ni Allaah, Uislamu ndio dini yangu."
Atapoulizwa "Wamtambuaje mtu huyu [Muhammad]?" Atasema "Alitujia
kwa haki tukamwamini na kumsadikisha." Atanadi Mwenye kunadi kutoka
mbinguni:
"Kasema kweli mja wangu, mfungulieni mlango wa Peponi na ajiwe na
harufu yake na aone mahala pake."
Kisha atajiwa na mtu mwenye nguo na uso mzuri, harufu nzuri. Atamuuliza
"Nani wewe, waonekana umekuja kwa khayr?"
Atasema:
"Mimi ni ´amali zako njema."
Atasema:
"Mola wangu simamisha Qiyaamah."
Ama kwa mtu asiekuwa muumini, atajiwa na mtu mwenye uso wakutisha,
nguo mbaya wakiwa na sanda kutoka Motoni. Kisha atajiwa na Malaika wa
kutoa roho na kumwambia:
"Ewe mtu mwenye nafsi chafu, toka uje kwenye ghadhabu na hasira za
Allaah”; roho itatoka kwenye mwili wake, wataivuta kama chuma cha Moto
kitokavyo kwenye pamba ziliolowa. Kisha wanaichukua na kuiweka kwenye
sanda ile, inatoka ikiwa kama kwamba ni harufu mbaya sana iliopatikana
katika uso wa ardhi. Watapanda nayo mbinguni ila hatofunguliwa milango ya
mbinguni, kisha kutasomwa:
"Na anayefedheheshwa na Allaah hana wakumhishimu. Hakika Allaah
Hufanya apendacho." (22:18)
Kisha Atanadi Mwenye kunadi mrudisheni katika ardhi:
"Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka
humo tutakutoeni mara nyengine." (20:55)
Atarudishiwa roho yake mwilini mwake, ajiwe na Malaika wawili wamuulize
kuhusu Mola wake, dini yake na Mtume wake? Atasema:
"Eeeh sijui! Nilisikia watu wakisema nami nikasema."
Allaah (Ta´ala) Katubainishia hali ya wanaokata roho kwa kusema:
"Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, basi ni raha, na manukato, na
Bustani zenye neema. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia." (56:88-91)
"Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, basi karamu yake ni maji
yanayochemka, na kutiwa Motoni. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. Basi
litakase jina la Mola wako aliye Mkubwa.” (56:92-96)
Adhabu na neema za kaburini ni jambo limetolewa dalili na Qur-aan na
Sunnah. Anasema Allaah (Ta´ala):
"Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya
dunia na katika Aakhirah." (14:27)
Wanasema wanachuoni Aayah hii inathibitisha adhabu na neema za kaburi.
Akasema tena Allaah (Ta´ala):
"Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapofika Saa ya Qiyaamah
patasemwa: “Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa!" (40:46)
Ni dalili kuwa wanaadhibiwa kwenye makaburi yao. Na Mtume (´alayhis-
Salaam) alipita kwenye kaburi mbili, akasema:
"Hakika hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa makubwa, Mmoja wao
hakuacha kujikinga na mkojo, ilhali wa pili alikuwa akisambaza uvumi.”
Na akasema:
“Adhabu nyingi za kaburi ni kuacha kujikinga na mkojo."
Na watu katika kaburi wanazidiana daraja. Katika kaburi kuna ajabu
miongoni mwa maajabu ya Allaah, hakuna neema wala adhabu zenye
kudumu. Na kuna wenye adhabu kisha kukaja neema, kadiri na hali za watu
zilivyokuwa duniani.
Adhabu ya kaburi ni haki isiokuwa na shaka, imetolewa dalili na Qur-aan na
Sunnah. Alikuwa Mtume (´alayhis-Salaam) akisema:
"Anapomaliza kusali mmoja wenu, amuombe Allaah kinga kwa mambo
manne kwa kusema: “Ee Allaah, mimi najikinga Kwako na adhabu za moto
na adhabu za kaburi na fitna ya uhai, na ya kufa, na shari ya [fitna] ya
Masiyhid-Dajjaal”."
Watu wa makaburi ndani ya makaburi yao watatamani fursa ya kufanya
´amali njema walipe. Imepokelewa kwa baadhi ya Salaf baada ya kufa kwao
wakiwaambia
"Nyinyi mnafanya ´amali na wala hamjui [yanayowasubiri], na sisi tunajua
na hatufanyia ´amali [hatuna fursa hiyo], hakika rakaa mbili za mmoja
wenu ni bora kuliko dunia na yaliomo ndani yake."
Hii kaburi ni kituo cha kwanza cha Aakhirah, ima itakuwa ni moja katika
Bustani za Peponi au moja ya shimo katika mashimo ya Motoni. Alisimama
´Uthmaan (radhiyallaahu ´anhu) kwenye kaburi moja, akalia mpaka ndevu
zake zikalowa.
Alipoulizwa, akasema: Nilimsikia Mtume (´alayhis-Salaam) akisema:
"Kaburi ndio kituo cha kwanza cha Aakhirah, ima ni moja katika Bustani za
Peponi au moja ya shimo katika mashimo ya Motoni."
Allaah (Ta´ala) Anasema:
"Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema." (82:13)
Neema katika dunia, na neema katika kaburi na neema siku ya Qiyaamah.
Watu watabaki kwenye makaburi katika hali zao mpaka Allaah
Ataposimamisha Qiyaamah.Israafiyl atapuliza parapanda.
"Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika
ardhi, isipokuwa aliyemtaka Allaah." (39:68)
Parapanda ambayo itauwa kila kiumbe, kisha kutapulizwa mara tena
wasimamishwe watu kwa Mola wa walimwengu, kisha kutapulizwa mara ya
mwisho watainuka wawe wanangojea. Anasema Allaah (Ta´ala): "Na
litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola
wao. Watasema: Ole wetu! Nani aliyetufufua kwenye makazi yetu? Haya
ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
Anasema Allaah (Ta´ala):
"Na litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa
Mola wao. Watasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye makazi yetu?
Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehemana wakasema kweli Mitume.
Haitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhurishwa mbele yetu.
Basi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale
mliyokuwa mkiyatenda." (36:51-54)
Anasema Mtume (´alayhis-Salaam):
"Vipi ntaimarika na alie na baragumu kaishika na anasubiri tu lini
ataamrishwa kuipuliza."
Mtu atasimama kwenye mizani yake akitetemeka hajui itakuwa na uzito au
itakuwa khafifu. Wakati wa kupewa vitabu, mtu hujui atapokea kitabu chake
kwa mkono wa kulia au wa kutosho. Na wakati wa kupita juu ya Swiraat, mtu
hajui ataokoka au hapana.
"Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, na mamaye na babaye, na mkewe na
wanawe; kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha."
(80:34-37)
Watasimamishwa watu kisimamo kirefu kizito kinachojua Allaah, kisha
watawaendea Mitume wa Allaah wakiwaomba wawaombee kwa Allaah
kutolewa katika hali waliomo. Watamuendea Aadam, Nuuh, Ibraahim,
Muusa, ´Iysa watakataa na kila Mtume atasema:
"Hakika Allaah leo Kakasirika ghadhabu ambayo Hajawahi kukasirika mfano
wake kabla."
Kila Mtume atasema "Ole wangu nafsi yangu, nendeni kwa mwengine."
Watamuendea imaam, bwana, mbora wa viumbe na Mitume Muhammad bin
´Abdillaah (swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Atasema mimi ndio mwenye
kuistahiki, na ndio maqaam al-Mahmuud aliomuahidi Allaah, kama
Alivyosema:
"Na amka usiku kwa ´ibaadah; ni ziada ya sunnah khasa kwako wewe.
Huenda Mola wako Akakunyanyua cheo kinacho sifika." (17:79)
Hakika kila Mtume alitanguliza maombi yake na Mtume kayaacha kwa
Ummah wake siku ya Qiyaamah. Ataenda na kwa unyenyekevu, amsifu na
amsujudie amuombe Allaah. Allaah Atamwambia "Inua kichwa chako, sema
utasikizwa, omba utapewa, ombea utakubaliwa."
Kisha Allaah Awahukumu waja wake:
"Je wanangoja mpaka Allaah Awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na
Malaika, na hukumu iwe imekwishatolewa? Na kwa Allaah ndio hurejeshwa
mashauri yote." (02:210)
Allaah Awatahesabu waja katika siku hiyo:
"Hakuna yeyote miongoni mwetu ila atamuongelesha Mola wake, hakuna
baina yake [Allaah] na baina yake mtarjumu; akiangalia kuliani kwake haoni
ila [mema] alioyatanguliza, kushotoni kwake haoni ila [maovu]
alioyatanguliza; akiangalia mbeleni kwake haoni ila Moto. Ogopeni Moto
walau kwa nusu tende."
Atamfanyia hesabu Allaah mja wake muumini na kumkumbusha mabaya
yake yote, kisha Mola wake Atamwambia nilikusitiri duniani na leo pia
nitamsitiri. Atawahesabu waja na kuwakariria na kuwatajia ´amali zao,
hawawezi wakayakataa. Wakiyakataa [waliyoyafanya] ni kama Alivyosema
Allaah:
"Leo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi
miguu yao kwa waliyokuwa wakiyachuma." (36:65)
"Na wao wataziambia ngozi zao: “Kwa nini mmetushuhudilia?” Nazo
zitasema: “Ametutamkisha Allaah Ambaye ametamkisha kila kitu, na Yeye
ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tumtarejeshwa”.”
(41:21)
Akikataa mja kukubali makosa yake, ataamrisha Allaah viungo vyake vitoe
ushahidi wa kila ´amali mpaka na ardhi aliokuwemo itashuhudia ima khayr
au shari:
"Siku hiyo itahadithia khabari zake." (99:04)
Kasema Mtume (´alayhis-Salaam):
"Khabari zake" ni kushuhudilia kila aliefanya juu yake [ardhi] ´amali ima za
khary au shari."
Allaah Atawafanyia hesabu waja, baadaye kutakuja kitabu cha kila mmoja
natija ya anaefanyiwa hesabu:
"Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale
yaliomo humo. Na watasema: “Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi
dogo wala kubwa ila huliandika?” Na watayakuta yote waliyoyatenda
yamehudhuria hapo. Na Mola wako hamdhulumu yeyote." (18:49)
"Na kila mtu tumemfungia ´amali yake shingoni mwake. Na Siku ya
Qiyaamah tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa.
Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu."
(17:13-14)
Vitabu vitagawiwa, kila mmoja atachukua kitabu chake ima atakichukua kwa
mkono wa kulia akisomea na kusema:
"Atasema: Haya someni kitabu changu! Hakika nilijua ya kuwa nitapokea
hisabu yangu. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza, katika Bustani
ya juu, matunda yake yakaribu. Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha
kwa sababu yamlivyo tanguliza katika siku zilizo pita." (69:20-24)
Kitabu chake atakishika kwa mkono wa kulia kwa enzi na saada. Kitabu cha
mafanikio hana shaka baada ya hapo, na neema haitomuondoka.
Kumeandikwa kwenye kitabu hichi:
"Bismillaahi Rahmaaniy Rahiym. Hichi ni kitabu kutoka kwa Mola wa
walimwengu, muingizeni fulani bin fulani Peponi..."
Hii ni neema na fadhila kubwa na natija nzuri kwa aliemuwafikisha Allaah
kumuimarisha na kujitahidi na akamuomba Allaah thabaat na Tawfiyq.
Asiekuwa muumini atakichukua kwa mkono wake wa kushoto au nyuma ya
mgongo wake huku akisema:
"Basi yeye atasema: “Laiti nisingelipewa kitabu changu! Wala nisingelijua nini
hisabu yangu. Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa. Mali
yangu hayakunifaa kitu. Madaraka yangu yamenipotea”." (69:25.29)
Hakuna yeyote ataingia Motoni ila atajua kuwa Moto unamstahiki kuliko
Pepo kutokana na uadilifu atauona kwa Allaah (Ta´ala).
Tunamuomba Allaah Usalama na afya. Ataezingatia kisimamo kama hichi
kikubwa, hali nzito, ataezingatia ukweli wa kukizingatia itamfanya azidishe
´amali njema; na kusimama na aliomuwajibishia Allaah juu yake, na
kukumbuka hali hizi iwe ni zawadi yake yeye ya kufanya ´amali njema kwa
yale Anayoyapenda Allaah na Kuyaridhia.
Chanzo: http://youtu.be/LuDeh8syfL4
Top Related