Web viewMwaka 2008 mwezi wa kwanza nilifanikiwa kuhamia Wilaya ya Hai na kupangiwa kituo cha kazi...
Transcript of Web viewMwaka 2008 mwezi wa kwanza nilifanikiwa kuhamia Wilaya ya Hai na kupangiwa kituo cha kazi...
HISTORIA YA MAISHA YANGU.
Mimi ninaitwa Benedicta Baltazari Swai. Nina umri wa miaka arobaini na nne, nilizaliwa
tarehe 10/10/1972 katika hospitali ya Huruma iliyoko Wilaya ya Rombo. Wazazi wangu
wanaishi katika kijiji cha Shimbi Mashariki katika Kata ya Shidehere Tarafa ya mkuu.
Nilipokuwa na umri wa miaka saba nilipata tatizo la kuugua macho kwa muda wa mwaka
mmoja na nusu. Wazazi wangu waliteseka na mimi sana hawakujua kama ningepona hivyo,
walinipeleka hospitali mbalimbali kwa matibabu. Madaktari waliposhindwa kunitibu wazazi
wangu waliamua kunipeleka kwa waganga wa kienyeji ili kunitibu tatizo langu waliahangaika
na mimi sana. Mwisho Mungu aliniponya wakamshukuru sana Mungu kwa macho yangu
kupona.
Mwaka 1981 nilianza elimu ya msingi katika shule ya msingi Kirokomu iliyoko Tarafa ya
mkuu Rombo niliendelea na masomo vizuri. Siku moja nilipokuwa darasa la sita tulipokuwa
tunacheza kwa bahati mbaya nilianguka na kuvunjika mkono wangu wa kulia nikapelekwa
hosipatalini kwa matibabu. Nilipata shida sana wakati wa masomo kwa kushindwa kuandika na
mkono wa kushoto. Baada ya miezi mitatu nilipona nikaendelea vizuri na masomo na kuhitimu
elimu ya msingi mwaka 1988. Badaye baba alinichukula fomu yakujinga na elimu ya sekondari
nikaijaza na kuchaguliwa na kuanza mafunzo hayo mwaka 1989 katika shule ya sekondari
Ibukoni. Niliendele na masomo vizuri shule yetu ilikuwa ni ya kutwa nilitembea kilometa tano
kutoka nyumbani hadi shuleni kwa muda wa miaka miwili baadaye ilikuwa na majengo ya
kulala wanafunzi nikaamua kuhamia. Niliendele vizuri na masomo, Siku moja wanafunzi
walifanya vurugu mbaya sana wakapiga nyumba za walimu kwa mawe, asubuhi yake tuliitwa
wote tulioko mabwenini na kupewa adhabu kali sana kisha tukaambiwa tuende nyumbani
tukawaite wazazi wetu. Wazazi walipokuja walimu waliita kamati ya bodi ya shule wakakaa
kikao kwa ajili ya kuzungumza tatizo hilo hatimaye kikao kiliamua shule ibaki ya kutwa.
Niliendelea na masomo vizuri na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1992
. Kwa bahati nzuri matokeo yalipotoka nilifaulu vizuri bali kutokana na shule yetu ilikuwa haija
sajiliwa siku bahatika kuendelea na masomo .
Hivyo, niliamua kuendelea na shughuli zangu za nyumbani, baadaye nilisika tangazo katika
vyombo vya habari kuwa kuna nafasi ya kujiunga na kozi ya ufundi na ukarani katika chuo cha
Moshi Community Centre. Niliposikia tangazo hilo nilichukuwa fomu ya maombi na kujaza
na kuituma baadaye nilichaguliwa kujiunga na kozi hiyo kwa miaka miwili. Nilianza mwaka
1994 hadi mwaka 1995 masomo niliyojifunza ni ushonaji, biashara, Kingereza, ofisi praktisi,
uchapishaji na Kifaransa. Nilihitimu tarehe 28/11/1995
.
Nilibahatika kuajiriwa katika kazi ya Ukarani na kupokea hela katika kiwanda cha mashine
yakukoboa na kusaga iliyoko mjini Moshi maeneo ya Mbuyuni Ostabey kwa tajiri yangu
aliyekua anaitwa Michael Mashele anayeishi jirani na mashine ya Mzee Gogo. Nilifanya kazi hii
kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwaka 1996 mwezi wa kwanza hadi mwaka 1998 mwezi
wa kwanza. Siku moja tulishindwa kuelewana na tajiri yangu aliye niajiri baada ya kutembelewa
na ndugu yangu anayeitwa Marietha alikua na shida nimpeleke kwa dada yetu anayeitwa Topista
aliyeolewa Kibosho Umbwe, kwani alikua ana mazungumzo naye. Nilimuomba tajiri yangu
ruhusa ili nimpeleke Kibosho kwani alikua ni mgeni kwa mazingira ya Moshi hivyo, haikua
rahisi kwenda mwenyewe na tajiri yangu hakukubali ndipo nikaamua kuondoka bila ruhusa,
niliporudi tajiri yangu hakuniruhusu kuendelea na kazi. Nilijitahidi kumuomba msamaha
ikashindikana lakini mke wake aliniomba nikae kwake ili kufanya shughuli za nyumbani
akaniahidi kunilipa mshahara wa shilingi elfu kumi kwa muda wa miezi mitano.
Mwezi wa kumi na mbili mwaka 1998 niliondoka baada ya kupata kazi kwa mama mmoja
Mzambia aitwae Mujanja, aliyeishi katika jiji la Arusha mtaa wa Kijenge eneo linaloitwa
Oloriani. Aliniahidi kunilipa mshahara wa shilingi elfu thelathini kwa mwezi mmoja. Shughuli
nilizokua ninazifanya ni kazi za ndani, na kuwalea watoto wake wawili wa kike. Mmoja jina lake
ni Twambo mwenye umri wa miaka 12 na wapili jina lake ni Nikay mwenye umri wa miaka tisa.
Watoto hawa hawakunipenda, kwani walinidharau sana, lakini mimi nilivumilia na kujitahidi
kuwaonyesha upendo wa dhati kwa lengo la kumtumikia kafiri ili nipate ujira wangu. Baada ya
muda wa mwaka mmoja nilishindwa kuendelea kuvumilia ndipo nilipo amua kuacha kazi na
kurudi Moshi kwa rafiki yangu Pelagia aliyekuwa anafanya kazi kwa mama Klementine
Foundation.
Mwaka 1999 mwezi wa kwanza nilipata kazi ya Ukarani kwenye Hoteli ya Pan Afrika na
mshahara wake ulikuwa wa shilingi elfu ishirini kwa mwezi mmoja. Bali nilifanya kazi bila
kulipwa mshahara inavyostahili, na badala yake alinilipa robo au nusu ya mshahara na wakati
mwingine kutokunilipa kabisa. Nilipoendelea na kazi ndani ya miezi sita bila malipo yoyote
niliamua kuacha kazi. Niliendelea kuishi kwa rafiki yangu anayeitwa Pelagia. Siku moja nilisikia
matangazo ya mkutano wa Injili uliokua unafanyika katika Kanisa la Tanzania Assemblies of
God la Amani lililoko Soweto Moshi.
Niliamua kuhudhuria huo mkutano na mwisho nilisikiliza neno la Mungu na kuamua kuokoka
na kumpa Yesu maisha yangu, mkutano ulipoisha niliamua kubatizwa Ubatizo wa maji mengi.
Niliamua kwenda kumsalimia mke wa tajiri yangu nilikokua nafanya kazi ya Ukarani kiwanda
cha mashine ya kukoboa na kusaga. Walinipokea kwa furaha sana baada ya kuwasimulia historia
ya maisha yangu walinishawishi kurudi kazini, na niliamua kukubali na kuanza kazi mwaka
2000 kwa muda wa miezi sita. Dada yangu anayeishi Kibosho anafanya biashara ya kuuza nguo
na viatu katika maduka yaliyoko jirani na Benki ya Nelson Mandela, siku moja alikuja
kumsalimia tajiri yangu na kuongea na mimi kwa kunishauri kuwa nikafanye kazi dukani kwake.
Nilikubali kuacha ile kazi ya mashine na kuanza kazi ya duka kwa muda wa miaka mitatu.
Nilisikia tangazo la nafasi za kujiunga na kozi ya mafunzo ya ualimu kwenye vyombo vya
habari mwaka 2003 mwezi wa kumi na mbili. Nilipo omba nafasi hiyo na kukubaliwa kwa kweli
nilimshukuru Mungu sana kwa kunipa nafasi hiyo. Mwaka 2004 mwezi wa kwanza ndipo
nilipoanza mafunzo ya ualimu daraja la tatu A katika Chuo Cha Ualimu kilichopo katika Mkoa
wa Kilimanjaro Moshi.
Niliendelea na masomo na kuhitimu tarehe 28 /11/2004. Baada ya hapo nilipata mchumba
anayeitwa
Annizeth Gasper Minde anayeishi Uru Mawela Mtaa wa Mamba. Ilipofika tarehe 3/3/ 2005
nilipangiwa kituo cha kazi kwa mafunzo ya ualimu uwanafunzi kwa vitendo kwa muda wa
mwaka mmoja, katika Mkoa wa Singida, Shule ya Msingi Mvae iliyoko Wilaya ya Singida
Vijijini na kuanza kazi 7/3/2005. Tarehe 18/12/2005 nilifunga ndoa ya Kikristo, katika Kanisa
la TAG Amani Soweto Moshi.
Mume wangu alikuwa anafanya kazi katika kiwanda cha KIBO MATCH kilichoko Magereza
Moshi Mjini. Baada ya usumbufu wa kutolipwa mshahara kwa muda mrefu aliamua kuacha kazi
na kuhamia Singida kwa shughuli za biashara, mwaka 2006. Niliajiriwa rasmi kwa cheo cha
ualimu daraja la tatu A tarehe 9/6/ 2007. Mungu alitujalia mtoto wa kike wa kwanza anayeitwa
Dorcas,
kweli tulifurahi sana kupata mtoto. Niliendelea na kazi kwa muda wa miaka minne huku
nikiendelea kuomba uhamisho wa kurudi Mkoa wa Kilimanjaro Moshi kutokana na mazingira ya
kazi kuwa magumu. Mwaka 2008 mwezi wa kwanza nilifanikiwa kuhamia Wilaya ya Hai na
kupangiwa kituo cha kazi katika shule ya Msingi Sere Ufundi iliyoko Machame Kaskazini na
kufanya kazi ndani ya mwaka mmoja. Mwaka 2009 nilipata uhamisho na kuhamia shule ya
msingi Ulali iliyoko Narumu na kufanya kazi ndani ya miaka mitatu. Tarehe 19/11/2010 Mungu
alitujalia mtoto wa pili wa kiume anayeitwa Joshua
tulimshukuru Mungu sana na kuendelea na kazi. Baadaye niliomba uhamisho na kuhamia Shule
ya msingi Kimashuku na kuanza kazi tarehe 22/1/2012. Lengo la kuhamia shule hiyo ni baada
ya mume wangu kuwa Mchungaji na eneo alilokua anafanya kazi kuwa mbali na eneo
ninalofanya kazi. Niliendelea na kazi kwa amani na kuishi vizuri na familia yangu kwa muda wa
miaka minne.
Baadae nilisikia tangazo katika vyombo vya habari kutoka NACTE la kozi ya mafunzo
ya Diploma ya ualimu kwa shule za msingi. Ndipo niliamua kushauriana na mume wangu na
kumsihi aendelee kuitunza familia ili mimi nikajiendeleze.
Mume wangu alipokubali nilichukua fomu ya kujiunga na Chuo cha ualimu Marangu na kuijaza
na mwisho kutuma maombi hayo kwa mtandao wa Intaneti kupitia NACTE, kwa katibu mkuu
wa Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kwa kuambatanisha vyeti ambavyo ni cheti cha
kuhitimu elimu ya sekondari na cheti cha kuhitimu mafunzo ya ualimu daraja la tatu A.
Nilijibiwa ombi langu na kuchaguliwa kujiunga na Chuo cha Ualimu Marangu tarehe 2/7/2015
na kuanza rasmi mafunzo ya Stashahada ya kawaida ya elimu ya msingi.
Katika Semista ya kwanza nilisoma masomo yafuatayo, English Literature, Stadi za Kazi,
Saikolojia, Stadi za Maisha, Hesabu na Sayansi. Nilifaulu vizuri Semista ya kwanza. Tarehe
02/11/2015 niliendelea na masomo ya Semista ya Pili hadi sasa yenye masomo nane ambayo ni
Hisabati, Historia, Jiografia, Siasa, Tehama, Upimaji, Mitaala na Kiswahili. Namshukuru Mungu
kwa kunijalia afya na nguvu yakuendelea vizuri na masomo yangu, na pia kuilinda familia yangu
nakuitunza vizuri. Pamoja na changamoto nyingi ninazozipitia za kifamilia na masomo kuwa
magumu bado sikati tamaa, ninatumaini la kuwa na ushindi mkubwa wa ufaulu wa masomo
yangu na pia ushindi mkubwa katika familia yangu kwani Bwana Yesu ni muweza wa yote.
Hivyo, ni matumaini yangu kuwa nitafaulu vizuri na kurudi katika kituo changu cha kazi
cha shule ya msingi Kimashuku. Pia ninamwomba Bwana Yesu anijalie uzima, afya njema,
nguvu, hekima, busara na akili njema. Ili niendelee kushirikiana vyema na wakufunzi wangu
vizuri katika kuhitimu elimu hii. Pia nawashukuru sana wazazi wangu walio nilea kwa malezi
mema, bila kuwasahau wakufunzi wote wa Chuo cha Ualimu Marangu, walimu wengine wote,
viongozi wa Dini, wadau na walezi mbalimbali katika kunipatia elimu mpaka nikaweza kufika
hapa nilipo. Mungu awabariki sana na kuwajalia maisha marefu na mazuri.