HALI YA TAALUMA YA UKALIMANI TANZANIA: JANA, LEO ... - Mwalimu Wa …€¦ · kuwasiliana kwa...
Transcript of HALI YA TAALUMA YA UKALIMANI TANZANIA: JANA, LEO ... - Mwalimu Wa …€¦ · kuwasiliana kwa...
HALI YA TAALUMA YA UKALIMANI TANZANIA: JANA,
LEO NA KESHO
Titus Mpemba
Ikisiri
Umuhimu wa ukalimani katika mawasiliano umeongezeka kutokana na utandawazi. Utandawazi
umerahisisha kukutanika na kuwasiliana kwa watu wazungumzao lugha tofauti kupitia wakalimani.
Kutokana na ongezeko hilo la umuhimu wa ukalimani, kumekuwa na jitihada mbalimbali katika
nchi mbalimbali kuhakikisha wanaandaliwa wataalamu wa kutosha kuendana na ongezeko hilo.
Hivyo, kumekuwa na ongezeko la tafiti katika uwanja huu na taasisi mbalimbali zimeanzishwa ili
kuandaa wataalamu wa fani hiyo na baadhi ya asasi zilizokuwapo zimepanua mafunzo yake na
kujumuisha programu za uzamili. Mathalani, mpaka kufikia mwaka 2011, Barani Ulaya peke yake
kulikuwa na takribani programu za mafunzo ya ukalimani kwa “ngazi ya umahiri zipatazo 135”
(Munday, 2008: 6). Mapinduzi haya, pamoja na kuendeshwa kwa makongamano mbalimbali na
kuchapishwa kwa machapisho mbalimbali kutokana na juhudi hizi, yameuwezesha ukalimani
kujichomoza na kusimama kama taaluma mahususi inayojitegemea (Garzone & Viezzi, 2002: 11).
Kwa kutumia mkabala wa kihistoria, makala haya yanachunguza jinsi nchi ya Tanzania ilivyoitikia
jitihada hizi za kukuza ukalimani na kufanya hivyo yatatathmini mafanikio, mbinu na changamoto
za jana na leo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kufanikisha harakati hizi hapo kesho. Makala
yanalenga kujibu maswali makuu matatu: (1) Ukalimani kama somo, ulianza kufunzwa lini nchini
Tanzania? (2) Hivi sasa taaluma ya ukalimani ina hali gani? na (3) Nini mustakabali wa taaluma
ya ukalimani nchini Tanzania?
1.0 Utangulizi
Umuhimu wa ukalimani katika mawasiliano ya siku za hivi karibuni umeongezeka
kutokana na utandawazi na kuongezeka kwa mwingiliano wa tamaduni mbalimbali
duniani. Katika zama hizi za utandawazi, kumekuwa na ongezeko la makutano ya
watu na tamaduni mbalimbali na haja ya watu hao—wazungumzao lugha tofauti—
kuwasiliana kwa sababu za kibiashara, kisiasa, kidiplomasia, kielimu, kidini na
masuala mengine ya kijamii. Hali hii imesababisha mwitiko wa namna mbalimbali
kutoka kwa watu wa nyanja mbalimbali duniani. Mathalani, watafiti wameongeza
zaidi juhudi za kuutafiti uwanja wa ukalimani kama anavyothibitisha Riccardi
(2002:15):
Tangu miaka ya 1950, wakati machapisho kuhusu ukalimani mikutanoni yalipotokea, utafiti
kuhusu ukalimani umefuata mikondo tofauti... (Herbert 1952; Rozan 1956; Paneth 1957).
Kwa mujibu wa uchambuzi wa data za kibibliografia uliofanywa na Pöchhacker (1995a),
idadi ya machapisho kuhusu ukalimani katika kipindi cha miaka 6 kuanzia 1989 hadi 1994
ilikuwa ni mara mbili ya yale ya miaka 36 iliyopita (1952 hadi 1988), hali inayoonesha
ushahidi bayana wa kuongezeka kwa raghba katika utafiti kuhusu ukalimani (Tafsiri ni
yangu).
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
113
Akimuunga mkono Riccardi huku akitilia mkazo kuhusu mwaka mmoja tu wa
2004, Pöchhacker (2011: 7) anaongezea kwa kusema:
Mwaka 2004 ni mwaka muhimu katika uchambuzi wowote wa maandiko
yanayohusu taaluma ya ukalimani. Mbali na ukweli kwamba ni mwaka wa
kuchapishwa kwa kitabu changu kitangulizi cha kiada ambamo mnapatikana
maelezo ya kina kuhusu chimbuko na maendeleo ya uwanja huu, na ambamo mna
mada nyingi kuhusu uga huu, kwa kuangalia idadi kubwa ya vitabu
vinavyoshughulikia ukalimani tu ambavyo vilichapishwa mwaka huo, mwaka 2004
unajichomoza kama mwaka wa miujiza ya utafiti kuhusu ukalimani (Tafsiri ni
yangu).
Licha ya ongezeko la tafiti, vilevile kumeanzishwa asasi na kozi mbalimbali kwa
ajili ya kufunza wakalimani katika ngazi mbalimbali (tazama Moser-Mercer, 2011:
49; Munday, 2012: 6).
Kwa jumla, wadau wa ukalimani katika nchi mbalimbali wameitikia kwa namna
tofautitofauti katika kukabiliana na ongezeko la umuhimu na mahitaji ya
ukalimani na wakalimani. Kwa kutumia mkabala wa kihistoria, makala haya
yanachunguza jinsi wadau mbalimbali wa ukalimani nchini Tanzania walivyoitikia
jitihada hizi za kukuza ukalimani ili kutathmini mafanikio, changamoto na mbinu
zilizotumika jana na zinazotumika leo na kutoa mapendekezo ya jinsi ya
kufanikisha harakati hizi hapo kesho. Kwa kuwa dhana yoyote kuhusu somo lolote
la taaluma mara nyingi hutegemea udhahanishi wa mtu anayejihusisha nalo
(Pöchhacker, 2004: 13), kabla ya kujitoma katika kujibu maswali tunayojiuliza
kuhusu ukalimani, makala yanaifasili kwanza dhana ya ukalimani; kisha, yanatoa
kwa ufupi historia ya ukalimani kuanzia kuibuka kwake hadi sasa. Hatimaye
makala yanatoa mapendekezo ya kuiendeleza taaluma ya ukalimani kwa manufaa
ya sasa na ya baadaye na mwisho ni hitimisho.
2.0 Fasili ya Ukalimani
Maandiko mengi yanayoifasili dhana ya ukalimani yanaonyesha kuwakilisha
mitazamo mitano na hivyo yanaweza “kugawanywa katika makundi matano”
(Pöchhacker, 2009: 133-134). Mtazamo wa kwanza unautazama ukalimani kama
aina mojawapo ya tafsiri. Mtazamo huu unawakilishwa na wanazuoni kama vile
Kade (1968), Setton (2002), Pöchhacker (2004 & 2009), Hale (2007), Bakize
(2013), miongoni mwa wengineo, na taasisi kama Longhorn (2011a) na TUKI
(2013), tukitaja kwa uchache. Mtazamo wa pili unauona ukalimani kama
mchakato wa kuzalisha vilongo au matini. Wanaosimamia mawazo haya ni pamoja
na Roy (2000) na Hale (2004), miongoni mwa wengineo. Mtazamo wa tatu
unauona ukalimani kama shughuli inayohusisha mchakato wa kiakili wa kuchakata
na kutoa taarifa. Wawakilishi wa mtazamo huu ni pamoja na Mshindo (2010).
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 114
Kundi la nne linautazama ukalimani kama upatanishi au uwezeshaji wa
mawasiliano baina ya pande mbili zinazotumia lugha tofauti. Katika kundi hili
kuna akina Nolan (2005) na Hatim (2009). Kundi la tano linauona ukalimani kama
jitihada za kutambua maana ya ujumbe na kuihawilisha kama ilivyo. Wawakilishi
wake ni pamoja na Seleskovitch (1968), Seleskovitch na Lederer (1989), Lederer
(1994), Seleskovitch na Lederer (1984/2001), na Israël na Lederer (2005), kwa
kutaja wachache tu.
Akiwakilisha mtazamo wa kwanza, Kade (1968), kama alivyorejelewa na
Pöchhacker (2004 & 2009), anaufasili ukalimani kuwa ni namna ya tafsiri ambapo
matini ya lugha chanzi huwasilishwa mara moja tu na hivyo haiwezi kupitiwa au
kurudiwa tena na ambapo matini ya lugha lengwa hutolewa katika mazingira
yenye shinikizo la ufinyu wa muda huku kukiwa na fursa finyu ya kufanya
masahihisho na udurusu. Akimuunga mkono Kade, Pöchhacker (2004: 11 & 2009:
133) anasema kuwa ukalimani ni “namna ya Tafsiri ambapo ufafanuzi wa
kwanza na wa mwisho kwa lugha nyingine hutolewa kwa kuzingatia
uwasilishaji wa mara moja wa usemi wa lugha chanzi” (tafsiri ni yangu lakini
msisitizo ni wake). Pöchhacker anafafanua kwamba anatumia neno “tafsiri”
linaloanza na herufi kubwa kwa maana yake pana. Anasema pia kwamba fasili
yake inachomoza kipengele cha upapo kwa papo.
Wakati Kade (1968) na Pöchhacker (2004) hawabainishi hali ya lugha
zinazohusika katika ukalimani kuwa ni ama mazungumzo, ishara au maandishi
kwa sababu wanachomoza kipengele cha upapo kwa papo, Longhorn (2011a) na
TUKI (2013), wakichomoza pia kipengele cha upapo kwa papo, wanazingatia
zaidi kipengele cha mazungumzo. Kwa mujibu wa Longhorn (2011a), ukalimani
ni “kazi ya kutafsiri maongezi au mazungumzo,” na kwa mujibu wa TUKI (2013),
ukalimani ni “kazi ya kufasiri papo kwa papo mazungumzo kutoka lugha moja
kwenda nyingine.” Maelezo ya Longhorn na TUKI kuwa kukalimani ni kutafsiri
mazungumzo yanashindwa moja kwa moja kutambua kuwa kuna ukalimani
unaotumia lugha za alama. Vilevile yanazibagua aina nyingine za ukalimani kama
ule wa soga za mtandaoni, upitishaji wa maandishi kwenye kiwambo cha runinga,
na ukalimani wa kutazamia ambapo mkalimani hutakiwa kuifafanua matini ya
kimaandishi inayokuwa mbele yake kwa lugha nyingine kwa njia ya uneni wa
papo kwa papo kadiri inavyosomwa katika lugha chanzi (Hale, 2007).
Ingawa kwa hakika wanazungumzia ukalimani, kwa kudai kuwa ukalimani ni aina
fulani ya tafsiri na kwamba ni kazi ya kutafsiri, Kade (1968), Pöchhacker (2004;
2009), Longhorn (2011a) na TUKI (2013) wanazitumia dhana za ‘ukalimani’ na
‘tafsiri’ kimtoano. Jambo hili tunadhani ni muhali kwa kuwa linazikanganya dhana
hizo na kuibebesha mzigo mzito dhana ya tafsiri. Pöchhacker (2004, 11)
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
115
mwenyewe anaelekea kukubaliana na madai haya anapoonesha wasiwasi fasili
yake kwa kusema, “Hata hivyo, kuiegemeza dhana yetu ya ukalimani katika
mawanda mapana ya Tafsiri kunatuweka katika mashaka makubwa ya jinsi ya
kuifasili dhana hii [ya Tafsiri].” Tunasema dhana hizi zinakanganywa kwa sababu
ukalimani na tafsiri, ingawa zina uhusiano wa karibu, ni taaluma mbili tofauti
zinazojitegemea. Garzone na Viezzi (2002: 11) wanathibitisha kuwa ukalimani ni
taaluma inayojitegemea wanaposema kuwa:
Ingawa utafiti wa ukalimani bado unatumia mikabala anuwai, wanazuoni
wanaojihusisha na utafiti huo sasa wanajitambua kwa kiasi kikubwa kuwa wako
katika jumuiya ya kiutafiti ambayo inajitegemea ... na inayoendelea kutambuliwa
kwa kiasi kikubwa na jumuiya ya kisayansi duniani (Tafsiri ni yangu).
Kukanganywa kwa istilahi za “ukalimani” na “tafsiri” kunaashiria kuwa licha ya
ukalimani na tafsiri kuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya binadamu (Schäfner,
2004: 1), watu wengi bado hawajui umahususi wa shughuli za mkalimani na za
mfasiri, jambo ambalo tunadhani litaswihi kudokezwa hapa kidogo. Nolan (2005:
2-3) anatutofautishia pande hizi mbili kwa kueleza tofauti tatu za msingi baina ya
shughuli za mkalimani na shughuli za mfasiri:
1. Mfasiri huchunguza taarifa iliyoandikwa kwa lugha moja (“lugha chanzi”)
na kuiwasilisha kimaandishi kwa lugha nyingine (“lugha lengwa”).
Mkalimani husikiliza ujumbe wa mazungumzo ulio katika lugha chanzi na
kuuwasilisha kwa mdomo katika lugha lengwa kwa njia ama ya ukalimani
andamizi au ukalimani sawia.
2. Mfasiri hutegemea utafiti wa kina, huku akiwa na nyenzo mbalimbali kama
maandiko kadha wa kadha na kamusi mbalimbali ili aweze kutoa tafsiri ya
kimaandishi iliyo sahihi na inayosomeka kwa usahihi kadiri
inavyowezekana. Mkalimani hutegemea uwezo wake wa kupata kiini cha
ujumbe na kukiwasilisha papo kwa papo kwa hadhira lengwa.
3. Shughuli ya mfasiri ni kama ile ya mwandishi, ilhali utendaji kazi wa
mkalimani ni kama ule wa mchezaji. Mfasiri mzuri anatumia muda wake
mwingi kutafuta istilahi sahihi ya kiufundi au uteuzi sahihi wa neno, lakini
mkalimani mzuri lazima aibuke papo hapo na ufafanuzi wa kuridhisha au
angalau kisawe kinachofaa iwapo neno sahihi halitamjia kichwani, ili
asisababishe hadhira yake kumsubiri kwa muda mrefu (Tafsiri yangu)
Hata hivyo, Schäfner (2004: 1), akiungwa mkono pia na Pöchhacker (2004: 10),
anaona kwamba kutofautisha ukalimani na tafsiri kwa kigezo cha maandishi, yaani
kwa kuona kuwa tafsiri huhusika na matini andishi na ukalimani huhusika na
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 116
usemi wa mazungumzo, ni mtazamo wa watu walei (wasio weledi) kwa kuwa
katika uwanja wa taaluma za tafsiri na mafunzo ya wafasiri na/au wakalimani
tayari kumeshafanyika jitihada za kueleza vigezo mahususi zaidi
vinavyozipambanua shughuli za pande hizo mbili. Akimrejelea Kade, Schäfner
(2004: 1-2) anachukua kigezo cha wakati kama msingi wa kuzitofautisha
shughuli za mkalimani na za mfasiri huku akikihusisha kigezo hicho na
upatikanaji wa matini chanzi. Anasema:
Kwa mfasiri, matini chanzi hupatikana katika muundo funge (kwa mfano, ikiwa
imechapwa katika karatasi au imerekodiwa katika kanda) mpaka pale matini lengwa
itakapokuwa imetolewa. Hali hii humruhusu mfasiri kuirejelea matini chanzi mara nyingi
kadiri inavyombidi ili kusahihisha na kudurusu matini lengwa, huku akitumia nyenzo
anuwai. Kwa hiyo, matini lengwa ya mwisho inaweza kuwa ni matokeo ya ‘majaribio’
kadhaa, ikiwa imetolewa ikipitia hatua kadhaa kuanzia rasimu ya kwanza hadi zao la
mwisho. Kinyume chake, mkalimani hupata jaribio moja tu la kutoa matini lengwa kama
zao la mwisho kwani matini lengwa huwasilishwa kwa mkalimani kwa mdomo na kwa
mara moja tu na matini lengwa haina budi kutolewa papo hapo. Hakuna uwezekano wa
kurejelea nyenzo na kuna fursa finyu ya kulifanyia masahihisho zao la mwisho.
Uwezekano wa kuhakiki uelewekaji wa matini chanzi na kusahihisha matini lengwa
hutegemea aina ya ukalimani: kwa mfano, inawezekana kuhakiki uelewekaji wa matini
chanzi kwenye ukalimani kiungo lakini si kwa ukalimani sawia ambapo mkalimani
hufanyia kazi kibandani. Hata kama matini chanzi itapatikana kwa mkalimani ikiwa katika
namna fulani ya mfumo funge (yaani nakala ya hotuba), matini halisi itakuwa ni hotuba
inayotolewa kwa mdomo (ambayo inaweza kutofautiana na ile iliyoandaliwa kimaandishi)
(Tafsiri yangu).
Kwa kuzingatia madai tuliyoyatoa hapo awali kwamba kitendo cha kutangaza
kuwa kukalimani ni kutafsiri mazungumzo kinazibagua aina kadhaa za ukalimani
kama ule wa kutumia lugha za alama na ule wa soga za mtandaoni, tunakubaliana
na Schäfner kuwa ni kweli kutumia kigezo cha maandishi na mazungumzo
kutofautisha ukalimani na tafsiri kina upungufu. Hata hivyo, tunaona kwamba
Nolan na Schäfner wanakamilishana zaidi kuliko wanavyotofautiana kama
tutakavyoonesha mwishoni mwa sehemu hii.
Tukiendelea na mtazamo wa pili, mwakilishi wa mtazamo huu, Roy (2000: 3-4),
anaufasili ukalimani kuwa ni mchakato wa kubadilishana mazungumzo kwa zamu
baina ya pande mbili zinazotumia lugha tofauti kwa njia ya mkalimani.
Wafuasi wa mtazamo wa tatu wanaufasili ukalimani kuwa ni shughuli
inayohusisha mchakato wa kiakili ambapo mkalimani huwa na jukumu la
kutambua, kuchakata na kutoa ujumbe wa kunenwa (Pöchhacker, 2009: 134).
Akiwakilisha mtazamo huu, Mshindo (2010: 30) anasema, “Ukalimani ni shughuli
ya kiakili inayowezesha kuwasiliana kwa maneno yanayosemwa au ishara
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
117
zinazooneshwa baina ya watu ambao hawasemi lugha moja, au ambao hawatumii
ishara za aina moja.”
Kwa mujibu wa mtazamo wa nne, ukalimani ni upatanishi au uwezeshaji wa
mawasiliano baina ya pande mbili au zaidi zinazotumia lugha tofauti na zenye
usuli wa tamaduni tofauti (Pöchhacker, 2008: 9-13; 2009: 134). Nolan (2005: 2)
anasema kwamba ukalimani unaweza kufasiliwa kwa ufupi kama uwasilishaji wa
uelewa kwa kuzingatia ukweli kwamba maana ya msemaji huelezeka vizuri zaidi
kwa lugha yake mama lakini hueleweka vizuri zaidi kwa lugha za wasikilizaji na,
kwa kuziba pengo la kimawasiliano baina ya lugha mbili au zaidi, wakalimani
huwasaidia wasemaji kutekeleza majukumu yao kwa kuwafanya waeleweke na
huwasaidia wasikilizaji kukidhi haja yao ya kuelewa yale yanayosemwa.
Wawakilishi wa kundi la tano, wanaufasili ukalimani kuwa ni jitihada za
kutambua maana ya ujumbe ambapo mkalimani hutakiwa kutoa ujumbe uliokitwa
kwenye uhawilishaji wa maana ya kauli nzima na si uhawilishaji wa maana ya
neno kwa neno ili kukidhi haja ya kimawasiliano ya pande zinazohusika katika
mawasiliano hayo (tazama Seleskovitch, 1968; Seleskovitch & Lederer, 1989;
Lederer, 1994; Seleskovitch & Lederer, 1984/2001; Israël & Lederer, 2005).
Mitazamo yote mitano hapo juu, tunaichukulia kuwa inakamilishana zaidi kuliko
inavyogongana. Kutokana na michango ya makundi yote matano, tunaweza
kubainisha vigezo mtambuka vinavyoweza kutusaidia kufasili dhana ya ukalimani
bila kuegemea mtazamo wowote mahususi. Vigezo hivyo ni pamoja na
upatikanaji wa matini chanzi, uchakataji wa ujumbe wa matini chanzi,
uzingatiaji wa utamaduni na muktadha, upapo kwa papo katika kutoa matini
lengwa, ufinyu wa fursa ya kuufanyia marekebisho ujumbe katika lugha
lengwa ukishatolewa, na lengo la mwisho ambalo ni kuwezesha mawasiliano
baina ya pande mbili zinazoshindwa kuwasiliana kwa sababu ya tofauti za lugha.
Kwa hiyo, kutokana na vigezo hivi, dhana ya ukalimani inaweza kufasiliwa kwa
upana kuwa ni “uwezeshaji wa mawasiliano baina ya pande mbili zinazotumia
lugha1 tofauti na zenye usuli wa tamaduni tofauti ambapo mwezeshaji hupokea
ujumbe wa matini ya lugha chanzi mara moja tu, huuchakata (huutafakari na
kuuelewa) na kisha kuuwasilisha kwa lugha nyingine papo kwa papo akizingatia
muktadha, sarufi na utamaduni wa lugha hiyo huku akiwa hana fursa ya kuufanyia
marekebisho.”
1 Tunalitumia neno lugha kwa maana yake pana inayojumuisha pia ishara zitumiwazo na watu
wasiosikia, yaani lugha ya alama.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 118
3.0 Hali ya Taaluma ya Ukalimani Nchini Tanzania: Jana, Leo na Kesho
Ukalimani unaelezwa kuwa ni desturi kongwe ambayo imekuwapo tangu kale
(Pöchhacker, 2004 & 2009; Giambruno, 2008; Baker & Saldanha, 2009) hata
kabla ya ugunduzi wa maandishi. Hata hivyo, ukalimani kama taaluma – elimu na
maarifa yanayopatikana kwa kusoma (Longhorn, 2011b) na kama mitalaa ya
utafiti – umeanza katika karne ya ishirini tu (Munday, 2008: 7; Pöchhacker, 2009:
129). Pöchhacker (2004) anaeleza kuwa shughuli hii imekua na kuendelea katika
vipindi mbalimbali vya kihistoria katika mazingira mbalimbali, tangu mazingira ya
kukutana kwa mara ya kwanza kwa makabila yanayotumia lugha tofauti hadi
kufikia hatua ya kuunganisha mataifa mbalimbali. Kwa kutumia mkabala wa
kihistoria, sehemu hii inayachunguza maendeleo hayo ya ukalimani, ikijihususisha
zaidi na nchi ya Tanzania. Tunaigawa historia ya maendeleo ya ukalimani nchini
Tanzania katika vipindi vikuu vitatu: jana (kabla ya na wakati wa ukoloni), leo
(baada ya ukoloni mpaka sasa) na kesho (siku zijazo). Katika kipindi cha jana,
tunaangalia hatua za mwanzo za ukalimani, yaani jinsi ulivyoibuka na kuendelea
nchini Tanzania. Tunaangalia pia jinsi ulivyostawi hadi kufikia hatua ya
kufundishwa kwenye mifumo rasmi ya elimu. Katika kipindi cha leo, tunaangalia
hali ya taaluma ya ukalimani ilivyo sasa na changamoto zinazoikabili. Na katika
kipindi cha kesho, tunaangalia mustakabali wa taaluma ya ukalimani nchini
Tanzania.
3.1 Jana
Kwa kuwa nyenzo kuu ya ukalimani ni lugha, kuibuka kwa ukalimani hakuna budi
kuhusishwa na kuzuka, kuanza kutumika na kuendelea kwa lugha. Ingawa
maandiko ya kidini yanaeleza kuwa Adamu alipoumbwa tu alipewa uwezo wa
kusema na kutoa majina kwa viumbe vyote vilivyokuwapo katika Bustani ya
Edeni (Mwanzo 2: 19-20), uhalisia unaonyesha kuwa binadamu anachukua muda
kujifunza lugha hadi kuwa na umilisi unaomwezesha kuitumia barabara. Utafiti pia
umeonesha kuwa ni takriban miaka kati ya 300,000 na 50,000 tu iliyopita ndipo
mwanadamu alianza kuwasiliana kwa kutumia lugha (Cobley, 2001; Holden na
wenzake, 2004; Yule, 2010). Ingawa mwanadamu alianza kutumia lugha miaka
mingi iliyopita, ni katika miaka ya karibuni tu ndipo ameanza kutumia huduma ya
ukalimani. Kwa mujibu wa Giambruno (2008: 27), “Kuna ushahidi wa kutumika
kwa wakalimani tangu miaka ya 3000KK huko Misri...” Ushahidi huo ni hiroglifu
na maandishi ya kwenye makaburi pamoja na marejeo ya kimaandishi
yanayoelezea majukumu muhimu ambayo wakalimani waliyatekeleza katika
Ugiriki ya Kale na Himaya ya Rumi. “Maandishi ya akina Caesar, Cicero, Horace,
Pliny na Valerius Maximus,” yote yanadokeza uhawilishaji wa ujumbe kutoka
lugha moja kwenda nyingine (Giambruno, 2008: 27).
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
119
Tukiacha nchi ya Misri inayotajwa kuwa ndipo ushahidi wa kale kuhusiana na
shughuli za ukalimani uliopatikana, utafiti wa wanazuoni wengi wa Kimagharibi
wanaochunguza maendeleo ya ukalimani unaelekea kuelemea upande wa nchi za
Magharibi na Asia peke yake (tazama, kwa mfano, Seleskovitch, 1968;
Seleskovitch & Lederer, 1989; Lederer, 1994; Seleskovitch & Lederer, 1984/2001;
Israël & Lederer, 2005; Pöchhacker, 2004 & 2009; Giambruno, 2008; Hatim,
2009). Hata hivyo, upo ushahidi kwamba ukalimani umekuwa pia ukiendelea
Barani Afrika kwa muda mrefu. Mathalani, Baker na Saldanha (2009: 313)
wanaeleza kuwa “tafsiri2 barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ina umri
takriban sawa na mawasiliano kwa njia ya mdomo.”
Utafiti wake ukiwa umejielekeza katika jamii ya Wahaya, Mutembei (2013)
anafafanua kuwa ukalimani ambao ulikuwa ukiendelea Barani Afrika kwa muda
mrefu, na ambao ungali ukiendelea, ni ule wa lugha za wahenga, au mizimu,
ambazo hunenwa na viti3 wao wanapokuwa wamepagawa. Barani Afrika, kabla ya
ujio wa dini za kigeni na ukoloni, wahenga walikuwa sehemu muhimu ya maisha
ya kila siku ya Waafrika. Kwa mujibu wa Mutembei (2013), kulipotokea matatizo
mbalimbali ya kijamii, kidini au kisiasa, Waafrika walitafuta ufumbuzi wa
matatizo hayo kwa wahenga. Wahenga hawa walikuwa wakiwasiliana nao kupitia
viti. Viti walipopagawa walizungumza lugha ambayo haieleweki bila msaada wa
mkalimani. Hivyo, ili lugha ya wahenga iweze kueleweka kwa watu wote
waliohudhuria tukio lililohusika, ilikuwa ni lazima isimbuliwe na mkalimani.
Ukalimani huu ungali ukiendelea katika jamii mbalimbali za Tanzania na Afrika
kwa jumla (tazama Beattie & Middleton, 1969; Wisjen & Tanner, 2002). Kwa hiyo,
mbali na eneo la jumla la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara linalotajwa na
Baker na Saldanha (2009), kuna ushahidi pia kwamba nchini Tanzania – ambayo
haikuwa na jina hili wakati huo – wakalimani walikuwapo hata kabla ya majilio ya
wakoloni.
Mbali na ukalimani wa lugha ya mizimu katika jamiilugha moja moja nchini
Tanzania, kulikuwapo pia na ukalimani baina ya watu waliozungumza lugha
tofauti katika biashara hasa ya kubadilishana vitu na mazao kabla ya ukoloni
(Pöchhacker, 2004; Hadjivayanis, 2011). Ingawa Pöchhacker (2004: 14) anadai
kuwa ukalimani wa kibiashara ndio wa kale zaidi, ukalimani wa lugha ya
mizimu unaelekea kuwa ndio ukalimani mkongwe kabisa kwani ulianza kabla
2 Baker na Saldanha wanatumia neno tafsiri kama istilahi ya jumla inayojumuisha pia ukalimani.
3 Wateule wanaopagawa na kutumiwa na wahenga kuzungumza ujumbe wao. Lugha wanenazo
wahenga hazieleweki kwa urahisi kwa watu wa kawaida. Hivyo, hukalimaniwa na watu maalumu
wanaoijua lugha ya kihenga.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 120
jamii hazijaanza kujihusisha na masuala ya biashara kati ya jamii moja na
nyingine.
Baadaye jamii zilistawi zaidi na kukazuka na kuimarika mifumo mbalimbali ya
kisiasa. Baadhi ya viongozi wa kisiasa wakaanza kubuni na kutumia lugha
maalumu ambayo haikueleweka kirahisi kwa watu wa kawaida. Hivyo, ilihitaji
kufafanuliwa na wakalimani ili watu wa kawaida waweze kuelewa. Wakimnukuu
Danquah (1928: 42), Baker na Saldanha (2009) wanafafanua kuwa wakalimani
hao hawakuwa na jukumu la kurudia tu maneno ya wakuu wao wakishasema kwa
lengo la kuyafanya yaeleweke kwa hadhira yote ya chifu au mfalme. Pia,
waliyadhihirisha kwa uwazi mamlaka ya mfalme yaliyokuwa katika kauli zake.
Aidha, wakalimani hao pia, walitarajiwa kuitia nakshi hotuba ya mfalme na
kufafanua dhamira yake kwa niaba yake. Baker na Saldanha (2009: 313-314)
wanaendelea kusema kwamba mkalimani hakutarajiwa kuongezea mada yoyote
mpya lakini alikuwa na ruksa ya kutanua semi za mfalme na kuzifuma upya
sentensi zake na kuichombeza hotuba kwa tafakuri za kicheshi na kifalsafa ambazo
zingempamba zaidi mfalme na mkalimani mwenyewe. Aidha, wanafafanua kuwa
jambo hili linathibitishwa na ukweli kwamba jamii za Kiafrika, Kusini mwa
Jangwa la Sahara kabla ya ukoloni, kama ilivyothibitishwa na utafiti wa
wanahistoria simulizi kama “Vansina, Bascom, Finnegan na Okpewho” na “baadhi
ya wamisionari na wapelelezi wa Kizungu”, zilikuwa zikihifadhi historia kichwani
na kuirithisha kutoka kizazi hadi kizazi kwa njia ya mdomo. Zilikuwa na watu
wenye vipaji vya kuhifadhi na kusimulia historia na utamaduni wa watu wao.
Hawa ndio walikuwa wakalimani na wafasiri wa wafalme, machifu na watemi
ambao walikuwa wakifanya kazi katika ikulu na mahakama ya himaya za kale za
Kiafrika. Hivyo, katika kipindi hiki ulizaliwa ukalimani wa kisiasa na ukalimani
wa mahakama. Hata hivyo, inafaa kudokeza hapa kwamba dhana ya mahakama
inayotajwa hapa ni tofauti na tunayoijua hivi leo.
Aidha, kufuatia kustawi kwa jamii na mifumo ya kisiasa kuzuka na kuimarika,
mbali na makutano ya wanajamii katika biashara, kuliibuka haja ya ushirikiano.
Viongozi wa kisiasa wa jamii zenye lugha tofauti waliweza kukutana na
kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa. Wakati mwingine viongozi
hawa walianzisha ushirikiano wa kisiasa baina yao. Jambo hili liliwezekana kwa
msaada wa wakalimani. Hata hivyo, wakati mwingine yalizuka mapigano baina
yao. Pöchhacker (2004: 14) anasema:
Pale wawakilishi wa jamii zenye lugha na tamaduni tofauti walipokutana kwa lengo
la kuanzisha na kuendeleza mahusiano ya kisiasa, ... walitegemea wawezeshaji wa
mawasiliano waliokuwa wakifanya ... ukalimani wa kidiplomasia. Pale mahusiano
yalipochacha, au pengine hata kabla hayajaanzishwa, migogoro ya kivita huenda
ililazimisha kuwapo kwa mawasiliano yaliyowezeshwa na wakalimani kwenye
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
121
mazingira ya kijeshi. Ukalimani wa kijeshi, kama unavyofanyika katika
mazungumzo na washirika, majadiliano ya kusitisha vita au usaili wa mateka, una
uhusiano wa kihistoria na ule wa kidiplomasia (Msisitizo ni wake lakini tafsiri
yangu)
Jamii zilivyoendelea kustawi, ziliendelea kujiimarisha na kupanua himaya zao,
huku jamii kadhaa zenye nguvu zikiziweka jamii dhaifu katika ukoloni na kuanza
kuwatawala. Kwa kufanya hivyo, ziliweka makundi ya watu mbalimbali
wanaosema lugha tofauti katika himaya moja. Katika hali kama hii, ili wakoloni
waweze kuwasiliana na watu waliowatawala na ili watu watawaliwa waweze
kupata huduma mbalimbali za kijamii, ilibidi ama watawala wajue lugha za
watawaliwa au watawaliwa wajue lugha ya watawala wao au pande zote zitegemee
huduma za wakalimani. Giambruno (2008: 29) anaeleza kuwa uvamizi mwingi na
mashambulio mengi katika mabara ya Asia, Afrika na Amerika ambayo
yalifanyika wakati wa ukoloni yalileta makutano ya lugha na kuhitaji ukalimani.
Aidha, kufuatia kuanzishwa kwa taasisi za kutekeleza sheria na kusimamia haki
katika maeneo mapya yaliyotekwa au yaliyowekwa chini ya ukoloni, wakalimani
waliandaliwa ili kuhakikisha kwamba hata watu wasiozungumza lugha ya
watawala wangeweza kuhudumiwa na kuwajibishwa pia. Hapo ukazaliwa
ukalimani mahakamani kwa dhana ya mahakama tunayoijua hii leo.
Wakati wa majilio ya ukoloni, wakalimani Tanzania walitumika kuwezesha
mawasiliano baina ya machifu na watangulizi wa ukoloni kama wamisionari na
wapelelezi waliofanya mikataba ya udanganyifu na katika daawa mbalimbali
mahakamani. Mathalani, mkataba uliotiwa saini baina ya mpelelezi wa
Kijerumani, Dkt. Karl Peters, na Sultani Mangungo wa Msowero huko Usagara
mnamo tarehe 29 Novemba 1884 unaeleza kuwa, “Mkataba huu umefafanuliwa
kwa Sultani Mangungo na Mkalimani Ramazan kwa uwazi na uangavu”
(Hollingsworth, 1929: 139). Akithibitisha kutumika kwa wakalimani katika
biashara kabla ya ukoloni na katika daawa mbalimbali mahakamani wakati wa
ukoloni, Hadjivayanis (2011: 2) anaeleza kuwa “lugha ya Kiswahili ilitekeleza
jukumu la ufasiri wa mdomo uliofanywa na wakalimani ambao walijulikana kwa
jina la mtapta4 wakati wa vipindi vya biashara za awali na halikadhalika katika
mahakama za kikoloni”. Whiteley (1969: 64) naye anaeleza kwamba “Hatimaye
hatua muhimu ilichukuliwa mnamo mwaka 1955 ya kuanzisha ukalimani sawia wa
Kiingereza/Kiswahili katika vikao vya Baraza la Kutunga Sheria.” Wakalimani wa
mwanzo wanaotajwa katika historia ya ukalimani Tanzania ni Ramazan ambaye
4Ingawa Hadjivayanis analitumia neno mtapta kuwakilisha dhana za mkalimani na mfasiri na
analitumia hivyohivyo hata anapozungumzia wingi, ufafanuzi wa neno hilo kwenye kamusi za
Kiswahili (tazama BAKIZA, 2010: 278; Longhorn, 2011a: 355; TUKI, 2013: 388) unaonyesha
kuwa lina maana ya mkalimani tu na kwamba wingi wake ni watapta.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 122
alikuwa mkalimani wa mpelelezi wa Kijerumani Karl Peters (Hollingsworth,
1929: 139), Selemani bin Mwenye Chande ambaye alikuwa mkalimani rasmi wa
Gavana wa Kijerumani wa Afrika Mashariki enzi za ukoloni wa Wajerumani
(Hadjivayanis, 2011: 22, akimrejelea Rollins, 1983: 50) na Kadhi wa Kilwa,
Mohamed bin Abdulrahman Hamdani ambaye alikuwa mkalimani wa
mahakamani aliyezungumza kwa ufasaha lugha za Kijerumani, Kiingereza,
Kiarabu na Kigujerati, pamoja na Brenn ambaye alikuwa mfasiri na mkalimani wa
kujitegemea (Hadjivayanis, 2011: 22-23).
Ushiriki wa Tanzania katika ustawi wa ukalimani ulioelezwa hapo juu,
unaonyesha kuwa baadhi ya wakalimani walioshiriki katika kuwezesha
mawasiliano wakati huo, walikuwa na maarifa mapana ya lugha, jambo ambalo ni
ishara kuwa huenda kulikuwa na mafunzo waliyoyapata kabla. Jambo hili linaibua
udadisi wetu na kutufanya tujiulize, “Ukalimani ulianza kufunzwa lini nchini
Tanzania?” Kwa mujibu wa Hadjivayanis (2011: 24), ukalimani ulianza
kufundishwa nchini Tanzania enzi za ukoloni wa Wajerumani. Wakati huo “Afrika
Mashariki ya enzi za ukoloni wa Wajerumani, ambayo ndiyo Tanzania ya sasa”
ilikuwa na shule zenye mfumo wa ngazi tatu. “Katika miaka mitatu ya kwanza,
wanafunzi walikuwa wakifundishwa kusoma, kuandika na kuhesabu.” Katika
ngazi ya pili, ambayo ilikuwa ni miaka miwili, “kulitolewa mafunzo ya ufundi” na
katika ngazi ya juu kulikuwa na shule moja iliyojengwa Tanga ambayo “ilitoa
mafunzo ya ukarani, kazi za viwandani na ualimu na halikadhalika baadhi ya kozi
za kitaaluma zilizolenga kuandaa ... wakusanya kodi, wakalimani, na mafundi...”
(tafsiri na msisitizo ni vyangu). Ingawa Hadjivayanis hataji mwaka mahususi,
historia inatuambia kwamba Shule ya Tanga ilijengwa mnamo miaka ya 18905.
Hivyo, kutokana na ukweli huu, tunaweza kuchukulia kwamba ukalimani ulianza
kufundishwa nchini Tanzania mnamo miaka ya 1890. Hata hivyo, tunadhani
wakati huo wakalimani walifundishwa tu kozi mbalimbali za lugha ambazo
ziliwapa stadi za kuwawezesha kukalimani lakini hakukuwa na programu
maalumu iliyokusudiwa kutoa wahitimu wenye utaalamu mahususi wa ukalimani
wenye astashahada, stashahada au shahada za ukalimani.
Ni vyema kukumbusha hapa kwamba mafunzo ya ukalimani ambayo tunasema
kuwa yalianza kutolewa miaka ya 1890 ni yale yanayofuata mfumo rasmi wa
elimu ya kuingia na kukaa darasani. Ukalimani uliofafanua lugha ya mizimu
tulioutaja hapo awali ulianza zamani kabla Tanzania haijaanzisha mahusiano na
watu wa mataifa ya nje kama Waarabu, Wajerumani na kadhalika. Wakati huo
5 Wilfred Whitely (1969) Swahili: the Rise of a National Language, ukurasa wa 59 anataja mwaka
1893 ilhali Abdi Mahboob na Ali Mahboob (2013) “Tanga Town: an Introduction” katika tanga-
line.tripod.com ( imseomwa tarehe 7 Novemba 2013) wanataja mwaka 1895.
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
123
elimu ilikuwa ikitolewa kwa njia ya mdomo, kuangalia na kwa kutenda na ilikuwa
ikirithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Wakalimani wa lugha ya
mizimu walipata elimu yao, kama wanavyoipata leo, kwa kurithishwa. Na elimu
hii haikuwa kwa kila mtu, bali watu wachache, mathalani, ukoo fulani tu.
Waingereza walipochukua nchi kutoka kwa Wajerumani, waliendeleza juhudi
zilizoanzishwa na Wajerumani. Wakoloni wa Kiingereza walitumia sera ya
utawala wa machifu ambayo ilikuwa “udongo wenye rutuba kwa ustawi wa
wakalimani” (Hadjivayanis, 2011: 23).
Pamoja na ukweli kwamba wakoloni walistawisha ukalimani Barani Afrika,
wakoloni wengine waliuviza kutokana na sera za tawala zao. Mathalani, wakati
ambapo wakoloni wa Kiingereza walitumia sera ya utawala wa machifu ambayo
iliruhusu kustawi kwa wakalimani, kama tulivyokwishaona, Wareno na Wafaransa
walipendelea sera ya usilimisho ambayo haikutoa fursa kwa lugha za kienyeji
kustawi (Baker & Saldanha, 2009: 316) na hivyo ilififisha ustawi wa ukalimani na
wakalimani.
3.2 Leo
Kuondolewa kwa wakoloni na kupatikana kwa uhuru katika nchi zilizokuwa
zikitawaliwa kulikuwa na athari kuhusiana na suala la ukalimani. Makundi ya
watu mbalimbali wanaosema lugha tofauti yaliendelea kuwekwa chini ya utawala
mmoja wa kisiasa kufuatia mipaka iliyowekwa na serikali za kikoloni na baadaye
kurithiwa na mataifa huru. Kwa sababu hii, huduma za ukalimani zimeendelea
kuwa tegemeo la watu wengi katika nchi zisizokuwa na lugha moja
inayowaunganisha wananchi wote, Tanzania ikiwamo. Leo hii, ukichochewa na
mahitaji ya utandawazi na utangamano wa kikanda, ukalimani umekuwa ni jambo
muhimu sana katika mawasiliano kwani watu wanaozungumza lugha tofauti sasa
wanaweza kufanya mikutano wakaelewana bila matatizo kwa msaada wa
wakalimani (Nolan, 2005). Hali hii, kama tulivyoeleza hapo awali, imesababisha
mwitiko wa namna mbalimbali duniani, kuanzia kupanuka kwa utafiti wa
ukalimani hadi kuanzishwa na kupanuliwa kwa mafunzo ya wakalimani katika
ngazi mbalimbali. Je, Tanzania imeitikiaje mapinduzi haya? Imekuwa na
mafanikio gani na inakabiliwa na changamoto zipi?
Baada ya kupata uhuru mnamo mwaka 1961, miongoni mwa mambo mengineyo,
Tanzania ilikipandisha hadhi Kiswahili. Ilikifanya kuwa lugha ya taifa mnamo
mwaka 1962. Na baada ya miaka miwili, kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1964,
Serikali ya Tanzania iliipandisha hadhi iliyokuwa Tume ya Lugha (ya Kiswahili)
ya Afrika Mashariki na kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Miongoni mwa
majukumu ya taasisi hii ni pamoja na kuandaa wakalimani na kutoa huduma za
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 124
ukalimani. Ingawa haijaanza rasmi kuandaa wakalimani, Taasisi hii tayari
imekwishaanzisha Kituo cha Istilahi, Tafsiri, Ukalimani na Teknolojia ya Lugha
kama namna ya kuitikia mahitaji ya huduma hii.
Aidha baada ya uhuru, Serikali ya Tanzania ilibadili mfumo wa elimu iliourithi
kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Mnamo mwaka 1967, Azimio la Arusha
lilitangazwa, Sera ya Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea ikatungwa na Kiswahili
kikatangazwa kuwa lugha ya kufundishia elimu yote ya msingi. Elimu ya msingi
ilitengewa miaka saba mfululizo. Wahitimu wengi walitazamiwa kwenda kuishi
vijijini na kutekeleza sera ya ujamaa na kujitegemea. Kwa hiyo, lugha ya
Kiswahili ndiyo iliwafaa zaidi. Kwa kuwa wahitimu wengi walitazamiwa kwenda
kuishi vijijini na kutekeleza sera ya ujamaa na kujitegemea, suala la ukalimani
halikutiliwa maanani katika mfumo huu mpya wa elimu. Elimu ya sekondari
iligawanywa katika ngazi mbili – ngazi ya kawaida na ngazi ya juu na ni
wanafunzi wachache tu ndio walitarajiwa kuendelea na masomo ya sekondari hadi
elimu ya juu. Ukalimani pia haukupewa nafasi katika elimu ya sekondari.
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ukalimani na masuala ya tafsiri, Serikali
ya Tanzania iliunda vyombo ambavyo, miongoni mwa mambo mengine, vilipewa
jukumu la kuratibu na kutoa huduma za ukalimani na tafsiri. Mathalani, mnamo
mwaka huohuo wa 1967 Bunge liliunda Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Miongoni mwa majukumu ya Baraza hili ni kuratibu na kutoa huduma za
ukalimani ndani na nje ya nchi ya Tanzania.
Kufuatia kuongezeka zaidi kwa mahitaji ya ukalimani na wakalimani, na kwa
kutambua kwamba msingi mzuri hujengwa kuanzia ngazi za chini, mnamo mwaka
2005 Serikali iliamua kuingiza vipengele vya masomo ya ukalimani na tafsiri
katika mtalaa wa elimu ya kidato cha tano na sita. Hatua hii imewahamasisha
waandishi na wataalamu wa Kiswahili kuandika vitabu vya ukalimani na tafsiri.
Mathalani, mpaka kufikia mwaka 2005 kulikuwa na kitabu kimoja tu cha tafsiri
ambacho kilikuwa kinatumika kwa wanafunzi wa somo la tafsiri katika vyuo
vikuu (tazama Mwansoko, 1996). Kitabu hiki hakina mada yoyote kuhusu
ukalimani. Hata hivyo, katika kipindi cha miaka minne peke yake kuanzia mwaka
2010 mpaka kufikia mwaka 2013, vitabu vinne vinavyoligusa suala la ukalimani
(tazama Mshindo, 2010; Wanjala, 2011; Haule & Tatinka, 2012; Bakize, 2013)
vimechapishwa. Pamoja na ongezeko la nyenzo hizi za kuandalia wakalimani na
wafasiri, hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa walimu wa somo la
Kiswahili kwamba vipengele hivyo vipya vya tafsiri na ukalimani vimeingizwa
bila ya wao kupatiwa mafunzo yoyote ya jinsi ya kufundisha maarifa hayo mapya
(tazama Bakize, 2013).
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
125
Katika kutekeleza majukumu yake, BAKITA limekuwa pia likiunga mkono juhudi
hizi za kuitikia mahitaji ya ukalimani na wakalimani. Mnamo mwaka 2007, kwa
mfano, BAKITA liliandaa warsha ya siku nne ili kutoa mafunzo kwa wakalimani.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wakalimani wasiopungua kumi, mwandishi wa
makala haya akiwa mmojawapo.
Aidha, viongozi wakubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia
wanatambua umuhimu wa fani ya ukalimani hivi sasa na wanafanya jitihada
mbalimbali kuhimiza vyombo vinavyohusika kuanzisha mafunzo ya ukalimani.
Kwa mfano, mnamo tarehe 27 Juni 2009, akizindua Taasisi ya Taaluma za
Kiswahili (TATAKI) – iliyokuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI),
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo
Pinda, alilithibitisha jambo hili aliposema: “Fani ya ukalimani ni muhimu hasa
wakati huu ambapo Kiswahili kinatumika sana katika mawasiliano ya viongozi wa
Serikali, katika mikutano na warsha mbalimbali zinazofanyika ndani na nje ya
Nchi.” Kwa kauli hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, hatuhitaji kusisitiza utambuzi
wa serikali kuhusu kuongezeka kwa umuhimu wa ukalimani na mahitaji ya
wakalimani. Hata hivyo, ni vyema tujiulize, “Je, ni hatua gani zaidi zimechukuliwa
kukabiliana na kuongezeka huko kwa mahitaji ya wakalimani na ukalimani?”
Kutokana na mabadiliko kadha wa kadha yaliyofanyika katika mataifa huru, mbali
na aina za ukalimani zilizokuwa zinatumika enzi za biashara ya kale na enzi za
ukoloni, aina nyingine za ukalimani ambazo hazikuwapo hapo awali zimeendelea
kujitokeza. Mathalani, suala la usawa wa binadamu limewashughulisha viongozi
wengi katika kuhakikisha kwamba wananchi wao wote wanapata ustawi na fursa
sawa katika huduma mbalimbali za kijamii, hali ambayo imesababisha aina
mbalimbali za ukalimani ziendelee kujitokeza na kustawi. Kwa mfano, sheria na
sera zinazotungwa ili kutoa fursa kwa viziwi kuwa na ushindani sawa na watu
wengine katika soko la ajira zimetoa msukumo mkubwa katika maendeleo ya
huduma za ukalimani kwa watumiaji wa lugha za alama (Pöchhacker, 2004: 14).
Kwa jitihada kama hizi, viziwi wamejikuta wakiingia katika mafunzo ya
kuwaandaa kuingia katika ajira na katika elimu kwa ujumla wake. Katika
mazingira kama haya, kumezaliwa ukalimani wa lugha ya alama katika elimu
(unaojulikana pia kama ukalimani wa kielimu). Tanzania imehakikisha watu
wenye matatizo ya kusikia hawaachwi nyuma. Kwa mujibu wa WASLI (2005)
kuna chuo kimoja cha walimu kinachoandaa walimu kwa ajili ya shule za watu
wenye mahitaji maalumu zipatazo nane na vitengo kwa ajili hiyo katika shule
nyingine za kawaida zipatazo 28 (tazama pia WFD & SNAD, 2008). Aidha,
kupitia vyombo kama Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) mafunzo kwa
wakalimani wa lugha ya alama yamekuwa yakitolewa. Kwa mujibu wa WASLI
(2005: 31), “Mafunzo ya majuma sita” hutolewa na CHAVITA kwa watu
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 126
wanaotaka kuwa wakalimani wa lugha ya alama ya Tanzania ambao hufanya
ukalimani katika shule mbalimbali.
Suala la ukimbizi na uhamiaji nalo limeibua mahitaji mapya ya kimawasiliano.
Watu wamekuwa wakizikimbia nchi zao kutokana na vita au majanga mengineyo
na kuhamia katika nchi zingine zinazozungumza lugha tofauti na za kwao. Hivyo,
ili wahamiaji hawa waweze kuishi vizuri katika nchi walimokimbilia na wapate
huduma za kijamii, kwa kuzingatia misingi ya upatikanaji wa fursa sawa kama
ilivyokuwa kwa viziwi katika soko la ajira, hakuna budi kuwe na huduma za
ukalimani katika taasisi anuwai za umma na huduma mbalimbali za kijamii. Kwa
hiyo, suala la uhamiaji limesababisha kuibuka kwa ukalimani wa kijamii,
“ambao pia unajulikana kama ukalimani katika huduma za umma (hasa nchini
Uingereza) na ukalimani wa kiutamaduni (nchini Kanada)” (Pöchhacker, 2004:
15). Ukalimani wa kijamii, kwa mujibu wa Pöchhacker (2004: 15) “umeibuka
kama uwanja mpya mpana wa shughuli za ukalimani, huku ukiwa na ukalimani
katika huduma za afya (ukalimani katika matibabu, ukalimani hospitalini) na
ukalimani wa kisheria kama nyanja muhimu zaidi za asasi.” Kwa mujibu wa
Chama cha Kimataifa cha Wakalimani Mikutanoni (maarufu kama AIIC (2013))6,
nchini Tanzania kuna wakalimani weledi wanachama wa chama hicho wapatao
kumi na sita walioko jijini Arusha wakifanya kazi ya ukalimani katika Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita Rwanda. Aidha, kutokana na uchache7 wa
wakalimani wa lugha ya alama, mbali na kutoa huduma shuleni, hufanya pia kazi
katika maeneo mengine ambapo huduma hiyo inahitajika. Nayo ni pamoja na
mikutanoni, hospitalini, mahakamani na runingani, kwa kutaja maeneo
machache tu. Akidokeza suala la wakalimani wa lugha ya alama Tanzania kufanya
kazi katika mazingira mbalimbali, Falconer (2003: 1 & 2) ana haya ya kusema:
… Hatimaye alikuwa mkalimani wa lugha ya alama Tanzania. Ndugu Singo amekuwa
mkalimani kwa miaka 6 sasa na amesafiri kwenda Uganda, Kenya, Uswidi … Msumbiji,
Zambia na Australia kukalimani mikutanoni ambako hufanya kazi kutoka Kiingereza
kwenda lugha ya alama ya Tanzania. Yeye [ndugu Singo] anawasiliana kwa ufasaha kwa
Kiswahili, Kiingereza na lugha ya alama ya Tanzania.
[Ndugu Singo] hupata pesa nyingi zaidi anapofanya kazi ya ukalimani kuliko
anapofundisha. Katika mazingira mengine, hata hivyo, ndugu Singo hukalimani bila
malipo kwa sababu anajua kwamba viziwi hawawezi kumudu [kulipia huduma hiyo kwa]
masuala ya binafsi kama harusi, mahakamani …, hospitalini, au katika chumba cha
6 http://aiic.net/directories/interpreters/city/1208/arusha
7 Idadi inayotajwa ni kati ya wakalimani 34 (tazama WASLI, 2011) na 45 (tazama WFD, 2008).
Hata hivyo, mkalimani mzoefu wa lugha ya alama Tanzania, Ndugu Geden Baulen Singo,
anasisitiza kuwa kuna wakalimani wa lugha ya alama Tanzania “watano tu” (tazama WASLI,
2007: 31).
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
127
kuhifadhia maiti – amewahi kwenda na ndugu kiziwi ili kutambua mwili wa
mwanafamilia. Kazi mbaya kuliko zote alizowahi kufanya ilikuwa kukalimani kwa
mwanamke kiziwi ambaye alikuwa anajifungua. Alifadhaishwa sana na hali hiyo (Tafsiri,
msisitizo na mabano mraba vyangu).
Aina nyingine ya ukalimani iliyoibuka katika kipindi hiki ni ukalimani katika
vyombo vya habari, au ukalimani matangazo. Ukalimani wa aina hii
unajidhihirisha zaidi kwenye runinga, na hivyo mara nyingi hutajwa kama
ukalimani runingani (Pöchhacker, 2004: 15). Nina hakika baadhi yetu
tumeshaona wakalimani wa lugha ya alama wakitoa huduma hii kwenye viwambo
vya runinga Tanzania. Aina hii kimsingi imebuniwa ili kuwawezesha watumiaji
wa vyombo vya habari ndani ya jamii kupata maudhui ya matangazo ambayo
vinginevyo hawawezi kuyapata kwa kuwa yanatolewa kwa lugha wasizozielewa.
Kwa mfano, lugha za kigeni, au lugha za kusemwa kama wanaotazama ni
watumiaji wa lugha za alama. Kwa upande wa lugha za kigeni, ukalimani huu
unaweza kufanywa kwa kupitisha maandishi kwenye kiwambo cha runinga; au
kwa lugha ya alama ili kuwawezesha watumiaji wa lugha za alama kupata habari.
Mambo mengine yaliyoibua aina mpya ya ukalimani ni utandawazi, utangamano
wa kikanda na maendeleo ya teknolojia. Tumekwishaeleza kuwa umuhimu wa
ukalimani katika mawasiliano ya binadamu kutokana na kuchochewa na mahitaji
ya utandawazi na utangamano wa kikanda, umeongezeka sana. Hii leo, kutokana
na mahitaji hayo na kufuatia maendeleo ya kiteknolojia, watu wanaozungumza
lugha tofauti kutoka pande mbalimbali za dunia wanafanya mikutano na
kuelewana bila matatizo kwa msaada wa wakalimani. Hivyo, mazingira haya
yameibua aina nyingine ya ukalimani inayojulikana kama ukalimani mikutanoni.
Kuna kampuni zisizopungua tano nchini Tanzania ambazo hutoa huduma ya
ukalimani mikutanoni. Idiomatic International Company Limited, Pinnacle
Interpretation Services, JHN Services Limited, Symposium International Limited
na Proficient Language Interpretation and Translation Services ni baadhi ya
kampuni yanayomilikiwa na Watanzania ambayo hutoa huduma ya ukalimani
mikutanoni.
Tunaona kwamba huduma za ukalimani kwa aina zote zilizoelezwa hapo juu
hupatikana katika nchi ya Tanzania. Ingawa huduma za ukalimani zinatolewa
nchini Tanzania, hali ya ukalimani kama taaluma bado hairidhishi nchini humo.
Akizindua TATAKI mnamo tarehe 27 Juni 2009, Waziri Mkuu wa Tanzania,
Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema, kauli ambayo aliirudia tena katika hotuba
yake ya kufunga mkutano wa tisa wa Bunge la Kumi uliofanyika mwezi Novemba
mwaka 2012, kwamba nchini Tanzania. “Hakuna chuo kikuu kinachotoa mafunzo
ya ukalimani. Watu wanaohitaji stadi hii ya ukalimani wanalazimika kwenda
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 128
kusomea katika vyuo vikuu vya nje ya Afrika Mashariki.” Maelezo haya ya Waziri
Mkuu ni ya kweli. Si tu kwamba hakuna chuo kikuu kinachotoa mafunzo ya
ukalimani bali hakuna chuo chochote kinachotoa mafunzo ya ukalimani.
Mathalani, kulingana na tovuti ya chama cha wakalimani mikutanoni
(www.aiic.net), kati ya asasi zaidi ya 508 duniani zinazohusika na mafunzo ya
wakalimani na kutoa programu za astashahada, stashahada na shahada zaidi ya 100
(tazama pia Munday, 2008: 6), ni taasisi tatu tu ndizo ziko Barani Afrika (mbili
zikiwa nchini Kameruni na moja ikiwa nchini Msumbiji). Tukiacha kozi mojamoja
ambazo mara nyingi huunganishwa kama tafsiri na ukalimani zikiwa ndani ya
programu za shahada za sanaa, lugha na ualimu, hakuna programu maalumu nchini
Tanzania inayotoa ama astashahada, stashahada au shahada ya ukalimani. Hata
hizo kozi zinazotolewa hazikidhi mahitaji kwani ni fupi na hazimpi mwanafunzi
fursa ya kubobea na kupata stadi stahiki zinazomwezesha kuwa mkalimani au
mfasiri mweledi. Kwa sababu taasisi za ukalimani ni chache, na idara nyingi za
serikali na vyombo vya habari havijaweka vitengo au idara za ukalimani,
wanafunzi hawapati fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika mazingira halisi
ya shughuli hizo. Aidha, walimu wengi wanaozifundisha kozi hizo si weledi wa
taaluma za ukalimani.
Kwa kuwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki hauna chuo kinachotoa mafunzo
ya ukalimani, tukiacha vyuo vilivyoanzisha kozi za ukalimani kama sehemu ya
programu za shahada nyingine, hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa. Mathalani,
kunahitajika kuanzishwa taasisi mahususi inayohusika na masomo ya ukalimani tu
ili wanafunzi wapikwe na kuiva barabara na wataalamu waliobobea katika uwanja
huu wapatikane.
Kama nchini Tanzania, na hata Afrika Mashariki yote, hakuna chuo kinachotoa
mafunzo ya ukalimani, je, wakalimani weledi basi tunao nchini Tanzania? Kama
tunao, je, hadi kufikia hivi leo wakalimani weledi waliopo ni wangapi na
wamefunzwa wapi? Pengine kabla ya kujitoma katika kuyajibu maswali haya,
ingeswihi kueleza tuna maana gani tunaposema “wakalimani weledi”. Weledi ni
hali ya kuwa na uelewa, ufahamu au ujuzi wa kina kuhusu kitu au jambo fulani
(Longhorn, 2011a & b; TUKI, 2013) unaotokana na kupata “mafunzo rasmi katika
uga” husika (Baker, 2012: 1). Kwa hiyo, wakalimani weledi ni wakalimani wenye
ujuzi wa kina kuhusu uga wa ukalimani ambao wameupata kutokana na
kuhudhuria mafunzo rasmi ya uga huo.
8 Idadi hii inahusu tu zile asasi zinazokidhi vigezo vya chama cha kimataifa cha wakalimani
mikutanoni (AIIC).
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
129
Tukirejea katika maswali yetu, si rahisi kupata vyanzo tunavyoweza kuvitegemea
na kusema kwa yakini kwamba wakalimani weledi tunao na idadi yao ni kadhaa.
Michuzi (2011), ingawa hatumii neno weledi, anadai kwamba wataalamu pekee
wa ukalimani wa kulipwa waliopo nchini Tanzania ni watatu. Nao ni David
Loserian, Gossaji Iddi Massoud, na Louis Taguaba ambao hutoa huduma katika
mikutano mbalimbali ya kimataifa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kireno na
Kihispaniola. Ingawa yeye hatumii neno weledi, kwa kuzingatia fasili ya neno
utalaamu kuwa ni elimu au ujuzi wa kiwango cha hali ya juu (Longhorn, 2011b)
katika jambo au fani maalumu (BAKIZA, 2010), tunaweza kudai kuwa hawa
wanaotajwa na Michuzi ni wakalimani weledi, na hivyo kuhitimisha kuwa
wakalimani weledi nchini Tanzania wapo.
Hata hivyo, kauli ya Michuzi kuwa hao wakalimani watatu aliowataja ndio
wataalamu pekee wa ukalimani wa kulipwa nchini Tanzania inatia shaka.
Kuna wakalimani wengine kama vile Ahmed Idarous, Donathila Mwaituka, Paul
Mwaituka, Valentine Karugaba, Imani Swilla na Mujawiri Mujawandu9, miongoni
mwa wengineo, watoao huduma ya ukalimani kwa malipo ambao Michuzi
hakuwataja. Shaka hii pia inathibitishwa na Chama cha Kimataifa cha Wakalimani
Mikutanoni (AIIC (2013)) ambacho kinasema kwamba nchini Tanzania kuna
wakalimani weledi wanachama wa chama hicho wapatao kumi na sita, wote
wakiwa jijini Arusha wakifanya kazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu
wa Kivita Rwanda (ICTR). Hawa hutoa huduma kwa lugha za Kiingereza na
Kifaransa tu. Majina yao yanatajwa kuwa ni Eli K. AMEMAVOR, Livinus
ATANGA, Aatsa ATOGHO, Emmanuel AYUK, Arlette BIKOK, Cheikh DIA,
Charles Diéne FAYE, Damian Atanga FONCHA, Kofi Elolo Sylvester
KUMODZI, Solange Balbine KENGUÉ TIOGO, Léontine MABIKA, Daniel
MBOUA YOGO, Emmanuel NDEH AVWONTOM, Justine Anastasie
NDONGO-KELLER, Edwin OCLOO-SEWOR na Oscar TANIFUM. Hata hivyo,
ingawa orodha hii ya AIIC ya wakalimani weledi nchini Tanzania ni ndefu,
inaonekana haihusishi Watanzania kwa kuwa wakalimani wote wanaotajwa
kwenye orodha hiyo wanaonekana kuwa ni raia wa Kameruni waliosomea fani ya
ukalimani katika Chuo Kikuu cha Buea nchini humo.
BAKITA, ambalo ni chombo cha Serikali chenye dhamana ya kuratibu na kutoa
huduma za ukalimani ndani na nje ya nchi, pia linakubali kwamba wakalimani
weledi wapo. Hata hivyo, lina shaka kuhusu idadi yao kamili. Mkuu wa Idara ya
Ukalimani na Tafsiri katika Baraza hilo anathibitisha jambo hili anaposema:
9 Mwandishi wa makala haya anawafahamu wakalimani hawa.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 130
Nimetakiwa … niijibu baruapepe … kuhusu kupatiwa inventory ya wakalimani
wanaotambuliwa na BAKITA na viwango vyao vya elimu. Kwa ujumla, nikuambie
tu kwamba hapa nchini kwetu wakalimani wanatoa huduma hiyo kwa uzoefu tu na
kwamba waliosomea hasa ukalimani na kupata vyeti ni wawili au watatu tu.
Nadhani hali hiyo unaielewa maana data hiyo tuliitoa wakati wa warsha yetu
(BAKITA) ambayo tuliifanya Kibaha wewe ukiwa mmojawapo wa washiriki. Idadi
ya wakalimani hao wanaofanya kazi kwa uzoefu inaweza kufikia 15. Hawa ni wa
lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kireno (Bi. D. Mwaituka, 3 Desemba,
2013, mawasiliano binafsi, msisitizo ni wangu).
Katibu Mtendaji wa BAKITA naye anaunga mkono madai ya Mkuu wa Idara ya
Tafsiri na Ukalimani anaposema:
Ukalimani, tofauti na tafsiri, hauna wataalamu hapa kwetu. Wataalamu
wanaoaminika ni Prof. Swilla (ambaye hakusomea fani hiyo) na Mzee Karugaba
(huyu sina uhakika kama kasomea au la). Mkalimani ambaye alikuwa amesomea
kabisa alikuwa hayati Prof. Magoti. Wengine ni wakalimani wa ridhaa ambao
kimsingi hawana diploma za fani hiyo. Donatila Mwaituka amesomea ukalimani
huko Msumbiji na ni mmoja wa wakalimani wachache wanaotumiwa na Umoja wa
Afrika katika mikutano na bunge lake … Kwa msingi huo sidhani kama kuna data
kubwa itakayopatikana katika eneo hilo (Dkt. S. Sewangi, 3 Desemba, 2013,
mawasiliano binafsi, msisitizo ni wangu).
Madondoo haya ni ithibati kwamba, kama tulivyodokeza hapo awali, si rahisi
kupata vyanzo tunavyoweza kuvitegemea kwa yakini kutupatia idadi kamili na
majina kamili ya wakalimani. Pengine kwa kuangalia majina ya wakalimani
weledi na wanaofanya kazi kwa uzoefu wanaotajwa katika madondoo hayo hapo
juu, pamoja na kumbukumbu za mwandishi alipohudhuria warsha inayotajwa hapo
juu na utafiti wake wa awali, tutaje kama kianzio cha mjadala majina machache
tunayoyakumbuka ya wakalimani Watanzania wanaofanyia kazi nchini Tanzania
(tazama jedwali la 1 hapa chini).
Jedwali la 1: Wakalimani wa Tanzania na Viwango Vyao vya Elimu ya Ukalimani
Na. Jina la
mkalimani
Kiwango
cha juu
cha elimu
Kiwango cha
elimu ya
ukalimani
Taasisi/Chuo
alikopatia
mafunzoya
ukalimani
Lugha
anazofanyia
kazi
1. Prof. Imani
Nitike Swilla
shahada ya
uzamivu
uzoefu - Kifaransa/
Kiingereza/
Kiswahili
2. Bw.
Valentino
Karugaba
shahada ya
umahiri
uzoefu - Kifaransa/
Kiswahili
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
131
3. Bw. Daniel
Mwaituka
shahada ya
awali
cheti cha tafsiri
na ukalimai
Chuo Kikuu
cha Eduardo
Mondlane,
Msumbiji
Kireno/Kiswahili
4. Bw. Titus
Mpemba
shahada ya
umahiri
uzoefu/mafunzo
ya siku nne
BAKITA Kiingereza/
Kiswahili
5. Dkt. Shani
Omari
shahada ya
uzamivu
uzoefu/mafunzo
ya siku nne
BAKITA Kifaransa/
Kiswahili
6. Bi. Donathila
Paul
Mwaituka
shahada ya
umahiri
cheti10
cha tafsiri
na ukalimani
Chuo Kikuu
cha Eduardo
Mondlane,
Msumbiji
Kiingereza/
Kireno/
Kifaransa/
Kiswahili
7. Bw. Ahmed
Idarous
shahada ya
umahiri
shahada ya
umahiri
Chuo Kikuu
cha Paris,
Ufaransa
Kifaransa/Kiinge
reza/Kiswahili
8. Bw. David
Loserian
shahada ya
umahiri
shahada ya awali Chuo Kikuu
cha Geneva,
Uswisi
Kifaransa/Kiinge
reza/Kiswahili
9. Daudi Sudi
Makabwe
shahada ya
awali
shahada ya awali Chuo Kikuu
cha Besançon,
Ufaransa
Kiingereza/
Kifaransa/
Kiswahili
10. Matthew
Kamba
stashahada uzoefu - Kiingereza/
Kiswahili
11. Bi. Judith
Prince
shahada ya
awali
cheti cha tafsiri
na ukalimai
Chuo Kikuu
cha Mtakatifu
Bonifasi,
Kanada
Kiswahili/
Kiingereza/
Kifaransa
12. Bw. Louis
Lwema
Taguaba
shahada ya
awali
uzoefu - Kifaransa/
Kiingereza/
Kiswahili
13. Bw. Mujawiri
Mujawandu
shahada ya
awali
uzoefu/mafunzo
ya siku nne
BAKITA Kiingereza/
Kiswahili
14. Bi. Hadija
Chipa
shahada ya
awali
uzoefu/mafunzo
ya siku nne
BAKITA Kiingereza/
Kiswahili
15. Bw. Geden
Baulen Singo
shahada ya
awali
uzoefu/mafunzo
ya majuma 6
CHAVITA Kiingereza/
Kiswahili/Lugha
ya Alama ya
Tanzania
16. Bw. Ibrahim
Mlosi
shahada ya
awali
uzoefu/shahada
ya
awali/mafunzo
ya majuma 6
Chuo cha
Imam Ali,
Syria/
CHAVITA
Kiingereza/
Kiarabu/
Kiswahili/Lugha
ya Alama ya
Tanzania
10
Vilevile amefanya utafiti juu ya ukalimani na kuwasilisha matokeo yake kwa kuandika tasnifu
iliyowasilishwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa minajili ya kukidhi matakwa ya
kutunukiwa Shahada ya Umahiri wa Kiswahili.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 132
17. Bw. Gossaji
Iddi Massoud
hatukufani
kiwa
kupata
taarifa
zake.
hatukufanikiwa
kupata taarifa
zake.
hatukufanikiwa
kupata taarifa
zake.
hatukufanikiwa
kupata taarifa
zake.
Chanzo: Data za awali kutokana na utafiti wa mwandishi
Kuna wakalimani wengine wanaotajwa katika tovuti mbalimbali ambao
hawakutajwa katika jedwali hili kutokana na kutokuwa na uhakika wa taarifa zao.
Mathalani, kuna wakalimani wapatao 13 wanaofanya kazi kwa uzoefu na
wakalimani 5 wenye vyeti wanaokalimani kwa lugha za Kiswahili, Kiingereza,
Kifaransa, Kireno, Kigiriki na Kikorea wanaorodheshwa katika
www.translatorstown/freelance-interpreters/tanzania. Tukiacha wakalimani
wanoonekana katika jedwali la 1 na wanaotajwa katika
www.translatorstown/freelance-interpreters/tanzania na tovuti nyinginezo, pia
kuna wakalimani wanaotoa huduma katika majukwaa ya kidini. Hawa pia hufanya
kazi kwa uzoefu tu na si rahisi kupata idadi yao kamili.
3.3 Kesho
Taaluma ya ukalimani inakua kwa kasi na wadau mbalimbali, kama
tulivyokwishaona, wanaitikia kwa namna mbalimbali ili kuendana na kasi ya
ongezeko hilo. Hata hivyo, ukalimani kama taaluma nchini Tanzania bado
unalegalega. Katika hali kama hii, tunajiuliza, “Nini mustakabali wa taaluma ya
ukalimani nchini Tanzania?” Ili kuweza kujibu swali hili hatuna budi kwanza
kubainisha ni changamoto gani zinazoikabili taaluma ya ukalimani nchini
Tanzania. Tunatakiwa pia kubainisha ni mambo gani yanayofanya taaluma
iendelee na istawi.
Hapo awali tulisema kuwa katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa tisa wa
Bunge la Kumi uliofanyika mwezi Novemba 2012, Waziri Mkuu wa Tanzania,
Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema kuwa nchini Tanzania hakuna chuo kikuu
kinachotoa mafunzo ya ukalimani na kwamba watu wanaohitaji stadi ya ukalimani
wanalazimika kwenda kuisomea katika vyuo vya nje ya Afrika Mashariki. Kwa
hiyo, changamoto ya kwanza ni ukosefu wa vyuo vinavyofundisha taaluma ya
ukalimani. Mbali na changamoto hii, Waziri Mkuu pia alibainisha kuwa:
Hata kama kukiwepo na wakalimani, bado hakuna kumbi za kisasa zenye vifaa vya
kusikilizia tafsiri za lugha mbalimbali. Kumbi nyingi tunazofanyia mikutano, tukiacha
Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC), hazina vifaa hivyo. Changamoto tuliyo nayo
kama Nchi na hasa wawekezaji wa kumbi za mikutano ni kuhakikisha kumbi zinazojengwa
na zilizopo zinakuwa na vifaa vya kutoa huduma ya ukalimani. Lengo ni kutumia fursa
hiyo katika kukuza lugha yetu ya Kiswahili.
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
133
Kwa hiyo, changamoto kubwa zinazoikabili taaluma ya ukalimani nchini Tanzania
ni pamoja na ukosefu wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya stadi hiyo na ukosefu wa
miundombinu inayowezesha kazi ya ukalimani kufanyika kwa ufanisi.
Kukosekana kwa vyuo vya ukalimani nchini, kumeikosesha Tanzania upendeleo
adhimu iliopewa na Umoja wa Afrika mwaka 2004 wa kupeleka wakalimani wa
Kiswahili wenye sifa ili waajiriwe na Umoja huo. Fursa hii imeharibika kutokana
na ukosefu wa vyuo vinavyohusika; na matokeo yake nchi imeendelea kupeleka
wabangaizaji wasio na sifa kielimu na kiumri11
.
Ili taaluma ya ukalimani iweze kuendelea na kustawi vizuri, kuna mambo kadhaa
yanayotakiwa kufanyika. Kwanza, kama tulivyoona hapo juu hakuna chuo cha
mafunzo ya fani hii, inabidi kuwe na taasisi zinazotoa mafunzo maalumu ya stadi
ya ukalimani. Akisisitiza umuhimu wa jambo hili katika ustawi wa taaluma
yoyote, Munday (2008: 6) anasema kuwa taaluma za tafsiri na ukalimani katika
nchi za Ulaya zimestawi na kuwa taaluma zinazojitegemea kwa sababu, miongoni
mwa mambo mengineyo, “kumekuwa na ongezeko kubwa la kozi zinazohusika
na tafsiri na ukalimani katika ngazi zote za shahada za awali na umahiri” ambazo
“zinaweka mkazo mahususi katika kutoa mafunzo ya wafasiri na wakalimani
weledi … na zinatumika kama kigezo aali cha kuwapokea wahitimu katika
ulimwengu wa wafasiri na wakalimani weledi”. Hata hivyo, ni vyema tukadokeza
hapa kwamba kuwapo kwa taasisi peke yake hakutoshi. Kunatakiwa pia kuwe na
miundombinu mbalimbali inayotakiwa na inayokidhi mahitaji ya kiwakati pamoja
na rasilimali muhimu zinazohitajika. Kwa mfano, mbali na miundombinu ya
kwenye kumbi za mikutano iliyotajwa na Waziri Mkuu hapo juu, katika uandaaji
wa wakalimani vyuoni kunahitajika pia madarasa mazuri, maabara bora, vitabu na
walimu wenye ujuzi. Kisha kunatakiwa kuwe na mazingira ya kuwapokea
wahitimu katika soko la ajira. Kwa mfano, vyombo vya habari, wizara za serikali,
na ofisi nyingine za serikali kama ikulu zinapaswa kuwa na vitengo vya ukalimani.
Kwa juhudi za vyuo kuanzisha kozi ya ukalimani katika mitalaa yao, tunaamini
kuwa mustakabali wa taaluma ya ukalimani utakuwa wa kutia matumaini kwa
kuwa ni kama umeanza kufunguliwa njia ya kusonga mbele. Jambo lililobaki ni
kuandaliwa kwa miundombinu ya kisasa na kuandaliwa kwa mazingira ya
kuwapokea wahitimu.
Jambo la pili linaloweza kusaidia ustawi wa taaluma ya ukalimani ni sera
zinazounga mkono juhudi ambazo zimeanza kuonekana katika taaluma hiyo.
Jambo hili linawezekana kama watunga sera watashawishika kuunga mkono
taaluma hii. Serikali ya Tanzania bila shaka inaunga mkono taaluma ya ukalimani
11
Taarifa hii ilitolewa na mtumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe nilipozungumza
naye mwezi Mei mwaka 2013.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 134
kama Waziri Mkuu, akizungumzia ukosefu wa taasisi zinazotoa mafunzo ya
ukalimani, anavyothibitisha anaposema, “Mimi najiuliza, hivi hili nalo tunalikubali
wakati lugha ni yetu? Ninaamini tunao uwezo wa kutumia vyuo vikuu na vyuo
vingine tulivyonavyo kufanya kazi hii ya kufundisha wakalimani. Ni vizuri vyuo
vyetu Nchini vianzishe Idara za Mafunzo ya Ukalimani ili kupunguza tatizo hilo.”
Kwa kauli hii ya Waziri Mkuu, inaweza kudaiwa kuwa milango iko wazi kwa
ustawi wa taaluma ya ukalimani kwani mazingira ya kisera yanaweza kuipa fursa
hiyo. Hata hivyo, tunadhani ingekuwa vizuri zaidi kama serikali ingeweka sera ya
kuvitaka vyombo vya habari, wizara za serikali na ofisi zingine za serikali kama
ikulu ziwe na vitengo vya ukalimani.
Jambo la tatu, ambalo limesaidia taaluma nyingi kustawi na kusimama kidete, ni
utafiti na uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huo katika makongamano mbalimbali
na uchapishaji wake katika majarida na vitabu. Munday (2008: 6) anashadidia
suala hili kwa kusema kwamba ustawi wa taaluma za ukalimani na tafsiri katika
nchi za Magaharibi umechangiwa na utafiti na “kuongezeka kwa makongamano,
vitabu na majarida kuhusu tafsiri kwa lugha mbalimbali” katika miongo miwili
iliyopita. Anataja, kwa mfano, majarida ya Babel na Target (ya nchini Uholanzi),
Meta na TTR (ya nchini Kanada), The Translator, Translation and Literature na
Translation Studies (ya nchini Uingereza), Across Languages and Cultures (la
nchini Hungaria), Cadernos de Tradução (la nchini Brazili), Perspectives (la
nchini Denmaki), Rivista Internazionale di Tecnica della Traduzione (la nchini
Italia), na Hermeneus, Livius na Sendebar (ya nchini Hispania). Kwa nchi ya
Tanzania, jambo hili bado ni changamoto. Hakuna hata jarida moja la ukalimani!
Hata majarida yaliyopo ya taaluma zinazohusiana na ukalimani kama vile isimu na
lugha, si rahisi kukuta makala ya ukalimani. Kwa upande wa vitabu, mpaka sasa
vitabu vinavyohusu ukalimani au vinavyogusia suala la ukalimani
vilivyochapishwa, kama ilivyokwishadokezwa, ni vinne tu. Utafiti uliojibainisha
kuhusu uwanja wa ukalimani ni tasnifu moja tu ya umahiri; ya kwanza kutokea
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (tazama Mwaituka, 2013). Kwa hiyo, ili
ukalimani ustawi nchini Tanzania siku zijazo, eneo la utafiti na uchapishaji wa
matokeo linahitaji kufanyiwa kazi zaidi.
Jambo la mwisho ni jumuiya za kitaaluma. Wataalamu wa ukalimani wanapaswa
kuwa na majukwaa ya kubadilishana mawazo katika ngazi ya kitaifa, kikanda na
kimataifa. Hivyo, wanapaswa kuanzisha vyama vya kitaifa na/au kujiunga na
vyama vya kikanda au kimataifa vya taaluma yao. Jambo hili litawaleta pamoja na
kuwaweka katika mtandao wa jumuiya nyingine zinazofanya kazi inayofanana na
yao. Akineneleza umuhimu wa jambo hili, Munday (2008: 6) anasema:
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
135
Jumuiya za kimataifa pia zimestawi. Jumuiya ya Fédération Internationale des
Traducteurs, iliyoanzishwa mnamo mwaka 1953 na Chama cha Wafasiri wa Kifaransa …
ilivileta pamoja vyama vya kitaifa vya wafasiri. Katika siku za karibuni zaidi, wanazuoni
wa taaluma za ukalimani wamejiunga pamoja kitaifa na kimataifa katika vyama kama
Association canadienne de traductologie (kilichoanzishwa huko Ottawa mnamo mwaka
1987), the European Society for Translation Studies (Vienna, 1992), the European
Association for Studies in Screen Translation (Cardiff, 1995) na the International
Association of Translation and Intercultural Studies (Korea, 2004) (Tafsiri yangu).
Nchini Tanzania kuna jumuiya moja tu ya wakalimani, nayo ni Chama cha
Wakalimani wa Lugha ya Alama Tanzania, ambayo inajulikana zaidi kwa jina lake
la Kiingereza la Tanzania Association of Sign Language Interpreters (TASLI)
iliyoanzishwa mwaka 2006 (WASLI, 2005). Kwa hiyo, ili kuistawisha taaluma ya
ukalimani nchini Tanzania, wanazuoni wa ukalimani wanahimizwa kuanzisha
jumuiya za kitaifa na kikanda na kujiunga katika jumuiya za kimataifa. Kwa
kufanya hivyo, tutaweza kuujenga mustakabali mzuri wa taaluma hii kwa miaka,
miongo au hata karne kadhaa zijazo.
4.0 Hitimisho
Makala haya yameabiri hali ya taaluma ya ukalimani nchini Tanzania.
Yameonesha kuwa umuhimu wa ukalimani katika mawasiliano siku za hivi
karibuni umeongezeka kutokana na utandawazi na kuongezeka kwa mwingiliano
wa tamaduni mbalimbali duniani, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa
utafiti wa ukalimani, kuanzishwa kwa asasi na kozi mbalimbali kwa ajili ya
kufunza wakalimani na miitiko mingine ya namna tofautitofauti. Kwa kuzingatia
mazingira hayo na kwa kutumia mkabala wa kihistoria, makala yametilia mkazo
jinsi wadau wa ukalimani nchini Tanzania walivyoitikia. Yamejaribu kujibu
maswali makuu matatu: (1) Ukalimani ulianza kufunzwa lini nchini Tanzania? (2)
Hivi sasa taaluma ya ukalimani ina hali gani? na (3) Nini mustakabali wa taaluma
ya ukalimani nchini Tanzania?
Tumeona kwamba ukalimani ulianza kufundishwa nchini Tanzania miaka ya 1890
wakati wakoloni wa Kijerumani walipojenga Shule ya Tanga ambayo “ilitoa
mafunzo ya ukarani, kazi za viwandani na ualimu na baadhi ya kozi za kitaaluma
zilizolenga kuandaa ... wakusanya kodi, wakalimani, na mafundi...” Kuhusu hali
ya taaluma ya ukalimani hivi sasa, imebainika kwamba aina mbalimbali za
ukalimani zimeendelea kuibuka na Tanzania haijabaki nyuma kuenda na wakati
kwani imeamua kuingiza vipengele vya masomo ya ukalimani na tafsiri katika
mtalaa wa elimu ya ngazi ya sekondari ya juu, hatua ambayo imewahamasisha
waandishi na wataalamu wa Kiswahili kama Mshindo (2010), Wanjala (2011),
Haule na Tatinka (2012) na Bakize (2013) kuandika na kuchapisha vitabu vya
ukalimani na tafsiri. Sanjari na juhudi hizi, vyombo vya Serikali kama BAKITA
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 136
vimekuwa vikiandaa warsha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakalimani na
viongozi wa Serikali wanahimiza vyombo vinavyohusika kuanzisha mafunzo ya
ukalimani. Imeelezwa pia kwamba asasi zisizo za kiserikali kama vile CHAVITA
zimekuwa zikitoa mafunzo kwa wakalimani wa lugha ya alama ili kuhakikisha
watu wenye matatizo ya kusikia hawaachwi nyuma. Pamoja na juhudi zote hizi,
imebainika kuwa taaluma ya ukalimani bado inalegalega kwa kuwa hakuna chuo
chochote kinachotoa mafunzo ya ukalimani Tanzania na ukanda mzima wa Afrika
Mashariki, hali ambayo imesababisha hata idadi ya wakalimani weledi na
wanaofanya kazi kwa uzoefu nchini isijulikane kwa yakini.
Ili taaluma ya ukalimani iendelee na kustawi Tanzania, unatolewa wito
kuanzishwe taasisi zinazotoa mafunzo maalumu ya taaluma ya ukalimani;
kuwekwe miundombinu mbalimbali inayotakiwa na inayokidhi mahitaji ya
kiwakati pamoja na rasilimali muhimu zinazohitajika; yaandaliwe mazingira ya
kuwapokea wahitimu wa ukalimani katika soko la ajira; zitungwe sera zinazounga
mkono ukalimani; ufanyike utafiti wa ukalimani, matokeo yawasilishwe katika
makongamano na yachapishwe katika majarida na vitabu; na wanazuoni wa
ukalimani waanzishe vyama vya kitaifa na/au wajiunge na jumuiya za kimataifa za
taaluma yao ili wawe na majukwaa ya kubadilishana mawazo.
Marejeo
AIIC. (2013). “Professional Interpreters by Language Pairs” kutoka
http://aiic.net/directories/interpreters/city/1208/arusha, imesomwa tarehe 5 Mei,
2014. Baker, Mona. (2012). In Other Words: a Coursebook on Translation, London na
New York: Routledge.
Baker, Mona na Saldanha, Gabriela (wah.) (2008) Routledge Encyclopedia of
Translation Studies 2nd Edition, Abingdon/New York/Canada: Routledge.
BAKIZA (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha, Nairobi: Oxford University Press
East Africa Ltd
Bakize, Leonard H. (2013). Tafsiri na Ukalimani kwa Shule za Sekondari, Dar
es Salaam: Leonard Herman Bakize.
Beattie, John na Middleton, John (wah.) (1969). Spirit Mediumship and Society in
Africa, London: Routledge & Kegan Paul.
Cobley, Paul. (2001). “Introduction” katika Cobley, Paul (mh.) The Routledge
Companion to Semiotics and Linguistics, London/New York: Routledge,
kur. 3-13.
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
137
Falconer, Kristi. (2003). “Profile of a Sign Language Interpreter from Tanzania,
East Africa” katika The AVLIC NEWS Juz. XIX No. 3 Julai 2003, Alberta:
the Association of Visual Language Interpreters of Canada, kur. 1-2.
Garzone, Giuliana na Viezzi, Maurizio. (2002). “Introduction” katika Garzone,
Giuliana na Viezzi, Maurizio (wah.) Interpreting in the 21st Century:
Challenges and Opportunities, Amsterdam/Philadelphia: John Benjamins
Publishing Company.
Giambruno, Cynthia. (2008). “The Role of the Interpreter in the Governance of
Sixteenth-and Seventeenth-century Spanish Colonies in the “New World”:
Lessons from the Past for the Present” katika Valero-Garces, Carmen na
Martin, Anne (wah.) Crossing Borders in Community Interpreting:
Definitions and Dilemmas, Amsterdam/Philadelphia: John Benjamins
Publishing Company, kur. 27-50.
Hadjivayanis, Ida. (2011). Norms of Swahili Translations in Tanzania: An
Analysis of Selected Translated Prose. Tasnifu ya Uzamivu, SOAS
http://eprints.soas.ac.uk/13602 imesomwa tarehe 31 Oktoba 2013.
Hale, Sandra B. (2007). Community Interpreting: Research and Practice in
Applied Linguistics, New York: Palgrave Macmillan.
Hale, Sandra B. (2004). The Discourse of Court Interpreting: Discourse Practices
of the Law, the Witness and the Interpreter, Amsterdam/Philadelphia: John
Benjamins Publishing Company.
Hatim, Basil. (2009). “Translating Text in Context” katika Munday, Jeremy (mh.)
The Routledge Companion to Translation Studies, London and New York:
Routledge-Taylor & Francis Group, kur. 36-53.
Haule, Festo C. na Tatinka, Feslas K. (2012). Nadharia ya Ukalimani: Sekondari
na Vyuo, Dar es Salaam: F. C. Haule.
Holden, Constance na wenzake. (2004). “The Origin of Speech” katika Science,
Washington DC: American Association for the Advancement of Science,
kur 1316-1319, www.science.org, imesomwa tarehe 27 Mei 2014.
Hollingsworth, Lawrence W. (1929). A Short History of the East Coast of Africa,
London: Macmillan and Co. Ltd.
Israël, F na Lederer, Marriane (wah.) (2005). La théorie interprétative de la
traduction, majuz. 3,Paris/Caen: Minard Lettres Modernes.
Lederer, Marriane. (1994/2003). La traduction aujourd’hui: Le modèle
interprétatif, Paris.
Hachette, kimefasiliwa na N. Larche kama Translation: The interpretive model
(2003), Manchester: St Jerome.
Longhorn. (2011a). Kamusi ya Karne ya 21, Dar es Salaam/Kampala/Nairobi:
Longhorn Publishers.
Longhorn. (2011b). Kamusi Kibindo ya Kiswahili, Dar es
Salaam/Kampala/Nairobi: Longhorn Publishers.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 138
Michuzi, Muhidin I. (2011). “Mabingwa wa Fani ya Ukalimani Tanzania” katika
issamichuzi.blogspot.com/2011/10/mabingwa-wa-fani-ya-ukalimani-
nchini.html?=1, imesomwa tarehe 3 Novemba 2013.
Mohamed, Mohamed A. (2011). Comprehensive Swahili-English Dictionary,
Nairobi/Kampala/Dar es Salaam/Kigali: East African Educational Publishers.
Mshindo, Hamad B. (2010). Kufasiri na Tafsiri, Zanzibar: Kiwanda cha Uchapaji
Chuo Kikuu cha Chukwani.
Munday, Jeremy. (2008) (toleo la 2). Introducing Translation Studies: Theories
and Applications, London na New York: Routledge-Taylor & Francis
Group.
Munday, Jeremy. (2012) (toleo la 2). Introducing Translation Studies: Theories
and Applications, London na New York: Routledge-Taylor & Francis
Group.
Mutembei, Aldin K. (2013). “Transcendental Language of the Bantu: the Case of
the Diviner-Mediums of the Haya People (Bahaya)” katika Legère, Karsten
(mh.) Bantu Languages and Linguistics: Papers in Memory of Dr. Rugatiri
D. K.Mekacha (Bayreuth African Studies Vol. 91), kur. 269-282, Bayreuth:
BASS.
Mwaituka, D. P. (2012). “Matatizo ya Kiutendaji katika Ukalimani wa Mikutano”
Dar es Salaam: Tasnifu ya Shahada ya Umahiri, Dar es Salaam
(Haijachapishwa).
Mwansoko, Hermus J. M. (1996). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu,
Dar es Salaam: TUKI.
Nolan, James. (2005). Interpretation: Techniques and Exercises,
Clevedon/Buffalo/Toronto:Multilingual Matters Ltd.
Pöchhacker, Franz. (2004). Introducing Interpreting Studies, New York/Canada:
Routledge.
Pöchhacker, Franz. (2008). “Interpreting as Mediation” katika Valero-Garces,
Carmen na Martin, Anne (wah.) Crossing Borders in Community
Interpreting: Definitions and Dilemmas, Amsterdam/Philadelphia: John
Benjamins Publishing Company, kur. 9 – 26.
Pöchhacker, Franz. (2009). “Issues in Interpreting Studies” katika Munday, Jeremy
(mh.) The Routledge Companion to Translation Studies, London & New
York: Routledge-Taylor & Francis Group, kur. 128-140.
Pöchhacker, Franz. (2011). “Researching Interpreting: Approaches to Inquiry”
katika Nicodemus, Brenda na Swabey, Laurie (wah.) Advances in
Interpreting Research: Inquiry in Action, Amsterdam/Philadelphia: John
Benjamins Publishing Company, kur. 5 – 26.
Riccardi, Alessandra. (2002). “Interpreting Research: Descriptive Aspects and
Methodological Proposals” katika Garzone, Giuliana na Viezzi, Maurizio
(wah.) Interpreting in the 21st Century: Challenges and Opportunities,
Hali ya Taaluma ya Ukalimani Tanzania: Jana, Leo na Kesho
139
Amsterdam/Philadelphia: John Benjamins Publishing Company, kur. 15 –
27.
Roy, Cynthia B. (2000). Interpreting as a Discourse Process, New York/Oxford:
Oxford University Press.
Schäffner, Christina. (2004). “Researching Translation and Interpreting” katika
Schäffner, Christina (mh.) Translation Research and Interpreting Research:
Traditions, Gaps and Synergies, Clevedon/Buffalo/Toronto: Multilingual
Matters Ltd, kur. 1 – 9.
Seleskovitch, Danica. (1968/1978). L’interprète dans les conférences
internationales: problèmes de langage et de communication, Paris: Minard,
kimefasiriwa (1978) kama Interpreting for International Conferences,
Washington, DC: Pen and Booth
Seleskovitch, Danica na Lederer, Marrianne. (1989). Pédagogie raisonnée de
l’interprétation, Paris: Didier Erudition.
Seleskovitch, Danica na Lederer, Marriane. (1984/2001). Interpréter pour
traduire, Paris: Didier Erudition.
Setton, Robin. (2002). “A Methodology for the Analysis of Interpretation
Corpora” katika Garzone, Giuliana na Viezzi, Maurizio (wah.) Interpreting
in the 21st Century: Challenges and Opportunities,
Amsterdam/Philadelphia: John Benjamins Publishing Company, kur. 29 –
45.
TUKI. (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam/Nairobi: Oxford
University Press.
Wanjala, Fred S. (2002). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri: kwa Shule, Vyuo na
Ndaki, Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
WASLI (World Association of Sign Language Interpreters) (2005) “Tanzania”
katika WASLI Country Reports 2005, Kampala: WASLI, uk. 31
WASLI (World Association of Sign Language Interpreters) (2011) “Tanzania
Country Report.” katika WASLI Country Reports 2011,
http://efsli.blogspot.com/2011/07/tanzania-country-report.html, imesomwa
tarehe 24 Mei 2014.
Whitely, Wilfred. (1969). Swahili: The Rise of a National Language. London.
Methuen and Co. Ltd.
Wisjen, Frans na Tanner, Ralph. (2002). ‘I am Just a Sukuma’: Globalization and
Identity Construction in Northwest Tanzania, New York: Editions Rodopi.
WFD (World Federation of the Deaf) na SNAD (Swedish National Association of
the Deaf). (2008) Global Survey Report. WFD Regional Secretariat for
Southern and Eastern Africa (WFD RSESA). Global Education Pre-
Planning Project on the Human Rights of Deaf People. Finland: World
Federation of the Deaf.
KISWAHILI JUZ. 76 (2013) 140
Yule, G. (2010). The Study of Language Fourth Edition, New York: Cambridge
University Press.